Kutoka kushoto ni Malkia wa Mipasho Afrika Mashariki Bi Khadija Kopa, Nasma Khamisi Kidogo (Marehemu), Bi Mwanahawa Ally na Khadija Yusuf .
Na Kado Cool
Mwanzoni mwa miaka ya 80, tuliokuwepo jijini wakati huo (baadhi yetu tukiwa vijana wadogo) tulishuhudia harusi nyingi zilizokuwa zikifanyika mitaani kwetu zikipambwa kwa wimbo maarufu wa "Kimasomaso" kutoka kwa Gwiji wa Taarab, marehemu Issa Matona.
Kwa wakati huo "Kimasomaso" ulikuwa kama wimbo wa Taifa wa harusi zote zinazofanyika jijini. Hakuna harusi iliyofanywa kwenye viunga vya Dar ikakosa kuwekwa wimbo wa "Kimasomaso" na kuonekana imekamilika.
Hii ni kutokana na wimbo huu kubeba ujumbe mahsusi unaotoa somo kwa wanandoa wote wawili katika maisha wanayoelekea kuishi. Hivyo "Kimasomaso" ulisaidia kutoa Usia kwa wanandoa kwa njia nyepesi sana wakati huo.
Nyakati hizi za miaka ya 80, utawala wa Taarab nchini ulikuwa chini ya kina Gwiji Issa Matona, Juma Bhalo, Shakira Said, Patricia Hillary na wengineo. Vikundi vya JKT, Bima Taarab, Muungano na vingine vingi vilionekana kushindana haswa.
Miaka ya 90 ikaingia na changamoto mpya. Enzi za "Kimasomaso" ya Issa Matona, "Pete" ya Juma Bhalo, "Nahodha" ya JKT Taarab, "Mapenzi Yananitatiza" ya Patricia Hillary zinaonekana kuanza kupokea upinzani mpya na mkali zaidi.
Kundi la Tanzania One Theatre (TOT) linaanzishwa na kutoa burudani mbalimbali kupitia Kwaya, Sarakasi, Maigizo na Taarab. TOT inaleta Joto jipya kwa vikundi vingine vya sanaa kama Muungano, Ujamaa, Makutano, DDC Kibisa, JKT nk.
Wasanii mahiri kama Khadija Omar Kopa, Nasma Khamis 'Kidogo', Fatma Ally 'Dogodogo' Ally Hemed 'Star', 'Profesa' Mohamed Mrisho, wakaleta Joto kali sana kwenye muziki wa Taarab. Vibao vyao vipya vikaonesha wamedhamiria kulishika jiji haswa.
Vibao vya "Ngwinji" kutoka kwa Khadija Kopa, "Nyama ya Bata" kutoka kwa Prof Mohamed Mrisho, "Kamba ya Mgomba" kutoka kwa Nasma Khamis, na "Zumbukuku" kutoka kwa Ally Hemed Star, viliifanya TOT kuingia kwa kishindo kikubwa kwenye tasnia.
Wakati haya yakiendelea, Muungano Culture Troupe maarufu kama "Madaktari wa Sanaa", walionekana kupambana haswa ili kulinda ufalme wao usiangushwe na kikundi kipya cha TOT ambacho kilionesha dhahiri kuliteka jiji la Dar na viunga vyake vyote.
TOT ikawa haishikiki haswa. Prof Mohamed Mrisho akaja na "Kijungu" huku Ally Star akitoa "Kukataliwa Kubaya" kabla ya Khadija Kopa kuzua taharuki na kibao chake cha "TX Mpenzi" kilichopigwa marufuku na serikali, kwa madai ya kutokuwa na lugha ya staha kwenye jamii.
Kiufupi, nyakati za miaka ya 90 zilikuwa na sura ya mapambano ya vikundi vikubwa viwili vya TOT na Muungano. Japo vikundi vingine viliendelea kutoa nyimbo zao mbalimbali, lakini 'upinzani wa jadi' uligeuka kuwa wa mafahari wawili, yaani Muungano na TOT.
Uhasama wa TOT na Muungano ukazidi kunogeshwa na hatua ya Muungano kumchukua Nasma Khamis kutoka TOT na hivyo kuleta 'uhasama' wa majibizano ya muda mrefu kupitia tungo zao.
Wakati Khadija Kopa akitoa kibao chake mahiri cha "Mambo ipo huku", hakutaraji wimbo wake huo kujibiwa na Nasma Khamis kupitia kibao cha "Mtu Mzima Hovyo" kilichogeuka mwiba mkali kwa Khadija Kopa.
Licha ya Khadija kujaribu kujibu wimbo huo kwa kutoa haraka kibao cha "Hujaambiwa wewe" lakini moto wa "Mtu Mzima Hovyo" ulionekana kushindwa kuzimwa na wimbo wowote mwingine uliotolewa wakati huo.
Wakati Khadija akiendelea kupambana kuifuta "Mtu Mzima Hovyo" kwenye vichwa vya watu kupitia kibao chake cha "Hujaambiwa wewe", Nasma naye akampa kubwa ya "Sanamu la Michelini" akimwambia 'hujaambiwa wewe vilevile Sanamu la Michelini...mbele huchezi, nyuma hutikisiki.!
Kuingia kwa Millennium mpya kukaja na joto lake. Kundi la Babloom Modern Taarab likatoa kibao kiitwacho "Asu" kilichoimbwa kwa umahiri na Abdul Misambano. Asu ikawa Asu kweli, kila mtu aliiimba na hivyo kuleta joto jipya katika muziki wa Taarab hususan kwenye viunga vya jiji la Dar.
Wakati Babloom wakilishika jiji na "Asu", vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars navyo vikaka katikati ya na kuleta ushindani mkali. Majina ya Sabah Muchacho, Mwanahawa Ally, Mwanamtama Amir, Afua Suleiman, Joha Kassim, Khadija Yusuph, Rukia Ramadhan, Mzee Yusuph na wengineo yakawa gumzo kubwa.
Vibao kama "Hakuna Tenda, Hakuna Buzi, Paparazzi" "Kinyago cha Mpapure", "Utalijua Jiji", "Zoazoa", "Tuliza Boli", "Paka Mapepe" na vinginevyo vilionekana dhahiri kuupa uhai mpya muziki wa Taarab nchini, uliyobatizwa jina la "Rusha Roho" wakati huo.
Niwakumbushe tu, nyakati hizi ndizo nyakati ambazo Bongo Fleva na Muziki wa Dansi vilikuwa juu sana. Ndizo nyakati za ubora wa Mr Nice, Prof Jay, Afande Sele, Lady Jaydee, TID, Jay Moe, Solo Thang, Gangwe Mobb, Juma Nature, Stara Thomas, Q Chief, East Coast Team na wengine kibao.
Ndizo nyakati ambazo Twanga Pepeta, TOT Band, Mchinga Sound, Chuchu Sound, Tamtam Band, FM Academia, Double M Sound, Beta Musica, Mokibo Sound, Mviko Sound, Mchinga Generation (G8), Extra Bongo, Double Extra na bendi nyingine nyingi zilikuwa hazishikiki.
Hizi ndizo nyakati za "African Bambataa" ya Clouds FM, chini ya marehemu Amina Chifupa, Othman Njaidi, marehemu Prince Baina Kamukulu, Boogie Master na Charles Mhamiji (Master C). Pia ndizo nyakati ya "Afro Rhythm" ya East African Radio chini ya Dj Mackey na Dj Fast Eddie.
Pamoja kuwa na foleni ya wanamuziki mahiri wa Bongo Fleva na Muziki wa Dansi wakiwa kwenye ubora wao, lakini bado muziki wa Taarab uliweza kula nao sambamba na hata kupora baadhi ya mashabiki wa Dansi na Bongo Fleva na kujikuta wakigeuka kuwa mashabiki wa Taarab.

0 Comments