Na Mwandishi Wetu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), CPA Ben’g i Issa amewataka vijana kuweka akiba na kuacha tabia ya kutumia zaidi ya wanachokipata.
Ben’g i Issa ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati akizundua Taasisi ya Chase Your Dreams, inayolenga kuwa mkono wa matumaini kwa vijana wa Kitanzania wanaopambana kufikia ndoto zao katika uchumi, elimu na ujasiriamali.
Alisema iwapo vijana wakizingatia uwekaji akiba na kutokutumia zaidi ya wanachopata, ni wazi kuwa watafanikiwa katika mipango yao, hivyo kutimiza ndoto zao.
“Ukipata elfu 10, tumia elfu 5. Usitumie kupita kipato unachopata, la sivyo utakopa kwa ajili ya matumizi, wakati mikopo ni kwa ajili ya kuendeleza biashara ama uwekezaji”.
Katibu huyo alisema ujio wa Taasisi ya Chase unaleta hamasa mpya ya maendeleo ya vijana, hivyo ni imani yake baada ya miaka mitano kundi kubwa la vijana litakuwa limefikiwa.
Beng’i alisema Taifa la Tanzania linaweza kupiga hatua kubwa kupitia kundi la vijana, hivyo ofisi yake itaweka kipaumbele kwenye kundi hilo.
Alisema mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa mpango, bidii na utekelezaji wa kile kinachowashinikiza ndani ya ndoto zao.
“Ukishakuwa na ndoto, lazima uwe na mpango wa kuifanikisha. Huwezi kuota na ukae. Ndoto hazijengwi kwa maneno, bali kwa vitendo na nidhamu.”
Kwa upande mwingine CPA Ben’gi amewataka vijana kujishughulisha na kuacha kukaa bure, kwani serikali imedhamiria kuwawezesha vijana, ikiwemo mpango wa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, kama ilivyotajwa katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassani wakati akifungua Bunge la 13.
Amewataka vijana wasiiogope dunia ya mafanikio, akiweka bayana kuwa maisha kuna kushindwa na kusonga mbele, hivyo wakifeli wainuke na wasiogope kufanya mambo makubwa.
Amefafanua kuwa uchumi ni nguzo muhimu katika heshima ya mtu kwenye jamii hata familia, kwa kuwa kukosa fedha huweza kumdhalilisha mtu kwenye ndoa, familia au katika mazingira ya kijamii.
Halikadhalika Katibu huyo amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa kwenye serikali, ikiwemo ununuzi wa umma kwa vikundi vidogo, mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, pamoja na kushiriki katika miradi mikubwa inayotekelezwa nchini..
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Lightness Makondo, alisema Chase Your Dreams ilianzishwa kutokana na changamoto zinazowakabili vijana wa Kitanzania kwa kushindwa kufikia ndoto kutokana na ukosefu wa elimu sahihi, rasilimali na uongozi wa kitaaluma.
“Kila kijana ana ndoto ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii. Ndoto isipotekelezwa inabaki kuwa maono yasiyo na dira.”
Alisema taasisi hiyo ilianza rasmi Machi 2024, ikiwa na program kuu tano ambazo ni After School Giving Program ambayo ilenga kutoa elimu na mwongozo kwa vijana waliomaliza shule ili kuwatengenezea dira ya maisha.
Alisema Program nyingine ni Mpango wa Kukuza Ujasiriamali ambayo inasaidia vijana kutambua fursa, kuanzisha biashara na kuzikuza kwa ujuzi sahihi.
“Pia tuna program ya Light Vikoba ambayo imejikita kwenye kuwekeza na kuweka akiba kwa vijana, ili kujenga misingi ya nidhamu ya fedha. Giving Back Program hii inarudisha kwa jamii kupitia miradi na huduma mbalimbali,” alisema
Alisema pia ipo program ya Kuwajengea Uwezo ambayo hadi sasa wamefikia vijana 1,200 ambao wamepata mafunzo ya elimu, ujasiriamali na usimamizi wa fedha.
Makondo alisema kuanzishwa kwa wizara mpya ya vijana kutakuwa daraja muhimu kati yao na vijana katika masuala ya uchumi, elimu na maendeleo.
Mkurugezni huyo alisema Chase ni mwanga mpya kwa vijana wa Kitanzania. “Ni mwaliko wa kuamka, kuchukua hatua, kuweka mipango na kutumia fursa zilizopo ili kujenga maisha bora, uchumi imara na taifa lenye nguvu ya vijana. Ndoto hazijengwi kwa maneno zinajengwa kwa vitendo, nidhamu, mipango, na ujasiri” alisema.
Naye Joanitha Jeremiah kutoka Visionary Youth Organization amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa faida, ikiwemo kujifunza, kufanya biashara na kujenga mitandao ya maendeleo, badala ya kupoteza muda kwa malumbano, matusi na kuonyesha maisha ya kuigiza.
Wakili Fredric Usiku amewataka vijana kuacha uoga kwani unachangia hasara kubwa sana. “Ukishindwa kufanya maamuzi, utashindwa kufika unapotaka.”
Alisema ili kuwa mjasiriamali mzuri, ni lazima ujitoe kafara, ajifunze, aongeze maarifa na awe jasiri wa kuchukua hatua.
Mbunifu wa Mavazi, Feith Debora amepongeza taasisi ya Chase kwa kuwa msaada kwa vijana, kwani kwa muda mrefu vijana wamekosa msaada kutoka kwa vijana wenzake.




0 Comments