MBETO AWASHANGAA PROFESA LIPUMBA, LUMUMBA WA KENYA


 Na Mwandishi Wetu, Zanzibar 

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeshangazwa na hatua ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Msomi mwenzake wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba kwa kuchomoza na kutafuta umaarufu unaopingana na ukweli wa mambo ulivyo. 

Vile vile chama hicho kimewakumbusha maProfesa hao kutumia elimu zao kwa kuwa wakweli na kuacha ushabiki wa kisiasa.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amemtaka Profesa Lipumba, kuacha janja yake ya kisiasa kwa lengo kuwadanganya waTanzania.

Mbeto alisema fikra na mawazo ya mwenyekiti huyo wa CUF ni yaliyokufa na yametolewa na mtu aliyechoka kisiasa hivyo jamii inapaswa kumtazama, kumsikiliza na kumpuuza.

Alisema kutaka matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 yafutwe, kisha iundwe Serikali ya Mpito ni kwenda upogo kwani Tanzania tayari ina Rais aliyechaguliwa na watu, ameshaapa kwa taratibu za kidemokrasia. 

"Profesa Lipumba nafikiri amechakaa kisiasa na kifikra. Ameshagota ukingoni hivyo apumzike awapisha wenzake wakiongoze CUF. Kutaka iundwe Serikali ya Mpito ni ishara ya kutapatapa ili ijitutumue kisiasa "aisema Mbeto.

Aidha alisema Mwenyekiti huyo hana haki wala ridhaa ya kuzungumzia dhana ya demokrasia , kwakuwa ndani ya chama chake anakabiliwa na tuhuma ya udikteta na kuwa king'ang'anizi wa madaraka.

 "Maelezo ya Profesa Lipumba kutaja Uchaguzi haukuwa huru, wazi na haki ni ulalamishi wa jikoni. Uchaguzi umeendeshwa kisheria kwa uwazi, haki na kidemokrasia. Kutaka serikali ya mpito ni ndoto za alinacha za mchana kweupe "alieleza.

Mwenezi huyo alisema, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ndio iliomtangaza Rais Dk Samia ameshinda Uchaguzi kwa Asilimia 98 baada ya kukamilika kwa njia za wazi na haki.

 "Nafikiri Profesa Lipumba ameanza kuzeeka kisiasa . amefilisika na hatoshi tena kusimama mbele ya wanasiasa wenzake. Amekuwa mgombea wa kudumu wa Urais toka Mwaka 1995 hadi 2020 .Arudi Kijijini kwake Ilorangulu akalime tumbaku " alisisitiza 

Hata hivyo, Mbeto akimzungumzia Profesa Lumumba, alimshauri msomi huyo angeweka mkazo wa kuishauri Serikali ya Kenya ambako kumekuwa na siasa za vuta, nikuvute kwa muda mrefu sasa.

Alisema Kenya kumetokea mivutano na tafran za kila aina lakini Profesa Lumumba sauti yake haikusikika hadi kufikia hatua ya Rais Dk William Ruto na aliyekuwa Makamo wake wa Rais Rigath Gachuaga kumfuta kazi .

Mbeto ,alisema ingekuwa hekima na busara kwa Profesa Lumumba akashughulika na matatizo ya nchi yake, kuzuka kwa ghasia za waandamanaji na jinsi ya kupata suluhu na muafaka wa ndani ya Kenya.

Post a Comment

0 Comments