Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema upinzani wa Zanzibar unachojua ni kupinga maendeleo kwasababu tu yemeletwa na Serikali ya Mapinduzi (SMZ
Kutokana na hali hiyo, hata kama zitajengwa barabara za dhahabu Zanzibar ACT watapinga.
Pia CCM kimekumbusha katika vitabu vitakatifu kuwa hata Nabii Yusuf alipingwa na makuhani wa Misri, aliposhika madaraka akiwa Mtendaji Mkuu wa dola ya kifalme huko Misri.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC ya CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis aliyesema mantiki ya kuwepo upinzani si kupinga na kubeza hata kwa mambo ya msingi.
Mbeto alisema anashangaa kuuona upinzani hususan ACT Wazalendo, bila aibu viongozi wake wamekuwa wakiipinga juhudi za maendeleo ya kisekta yanayoonekana.
"SMZ chini ya CCM, hata ikijenga barabara za dhababu , Majengo ya shule kwa kutumia matofali ya almasi na lulu, ACT kitabeza na kuita huo ni mkaa wa kuni za mikarafuu" .
Mbeto alikitaja kitendo cha upinzani kupinga kila jambo la maendeleo hakikuanzishwa na ACT kwani hata wahafidhina wa wakati huo, walipinga maendeleo yaliyokuwa yanaletwa na Afro Shirazi Party (ASP), chini ya Rais wa kwanza, hayati Abeid Amani Karume pia walimpinga alipoleta maendeleo .
"Maendeleo hayakuwepo Zanzibar enzi za ukoloni. Bila aibu vibaraka na wapinga maendeleo dhidi ya serikali ya ASP hawakuacha kubeza" alisema.
Mbeto alibainisha kuwa wapinzani wa ASP walidai SMZ haijafanya lolote licha ya juhudi kubwa alizokuwa akifanya hayati Karume kuwaondoa waZanzibari katika umaskini.
Katibu huyo Mwenezi alisema hata Nabii Yusuf alipingwa na wapinzani wake asifanikishe sekta ya kilimo cha umwagiliaji na kujenga maghala hivyo ACT kinapopinga maendeleo ni asili ile ile ya upinzani.
'Makuhani wa Misri walimbagua Nabii Yusuf wakidai hana asili ya Misri. Wakamwita mshamba toka kijijini Canaan huko Palestina.
Akafayiwa vituko akwame kuleta maendeleo lakini alisimama imara akabadili Misri kwa muda mfupi na ndio maana toka wakati huo hadi sasa Misri hakuna njaa" alisema.
Katibu Mwenezi huyo alisema kwa bahati nzuri wananchi wa Zanzibar wameshapevuka kifikra na kupata mwamko wa maendeleo hivyo wanajua kutofautisha ukweli na porojo za wanasiasa uchwara.
"Wananchi wameshuhudia shule za ghorofa zikijengwa, barabara, masoko, viwanja vya ndege, bandari na madaraja yakijengwa. Wanajua kutofautisha kati ya maendeleo na porojo za kisiasa za majukwaani" alieleza.
Mbeto alisema Mzee
Karume alipotekeleza malengo ya ASP na ya kimajumui hatimae Tanganyika na Zanzibar zikaungana, alichekwa na wapinzani wake.
Katibu huyo Mwenezi alisema tabia ya kupinga kila kitu imekuwa mila, desturi na utamaduni kwa upinzani wa Zanzibar ambao pengine wangependa wananchi wabakie kwenye dimbwi la ufukara huku wakikosa huduma muhimu za elimu, afya na wakiwa hawana fursa zozote za kujikwamua kiuchumi.

0 Comments