DKT. MWINYI BILA AMANI HATA IBADA TUTASHINDWA

 

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM ambaye pia ni Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi alisema amani tunu bila kuwa nayo hata ibada watu watashindwa kufanya.


Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika, Tumbatu Uvivin, Dkt. Mwinyi aliwataka wananchi hao wasiruhusu mtu yeyote kuvunja umoja wa waZanzibari uliojengeka ndani ya miaka mitano ya utawala wake.

"Msingi uliopo katika sera ya Ilani ya CCM ni kudumisha amani, umoja, mshikamano na kuondoa ubaguzi" alisema na kuongeza kuwa kama wanataka maendeleo wachague CCM.

Aliwataka wasiwasikilize ambao hawana sera isipokuwa ubaguzi miongoni mwa waZanzibar.

"Mzanzibari yeyote anaweza kuwa na nasaba na Tanzania Bara, Oman, India wote wanapaswa kuwa na umoja" alisema.

Mgombea huyo wa Urais kwa kipindi cha pili alisema, wakati anaomba kura kipindi kilichopita aliombwa huduma za jamii.

 " Niliombwa hospitali, tunajenga ya wilaya itakayokuwa na huduma zote muhimu ikiwa ni upasuaji ujenzi wake unaendelea na karibuni itakamilika" alisema.

Alisema anajua changamoto ya watoto kusoma kwa awamu zaidi ya mbili na ndio maana imejengwa shule ya ghorofa yenye vyumba vya kutosha vya madarasa.

Alibainisha kuwa awamu ya pili ya mikopo inayoenda kutolewa ni ya boti kubwa kwa wavuvi wadogo ili waweze kufika mbali zaidi na kupata samaki wengi hivyo kupata tija zaidi.

Post a Comment

0 Comments