TAFF YAKABIDHI ZAWADI KWA WASHINDI

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu (Taff) limezikabidhi zawadi kwa timu zilizofanya vizuri katika mashindano ya soka yaliyofanyika Azam Complex Chamazi Dar es Salaam yakishirikisha timu nane.

Timu zilizokabidhiwa zawadi ni bingwa Ubungo FC ambayo imeondoka na Sh milioni moja, mshindi wa pili Sauti Parasports Sh 500,000 na mshindi wa tatu Arusha Warriors Sh 250,000.

Kadhalika kila timu iliyoshiriki pamoja na kugharamiwa usafiri, malazi na chakula imepatiwa Sh 400,000.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi zao nahodha wa Ubungo FC, Frank Ngairo na Ashraf Alombile wa Sauti Parasports walishukuru kwa kupatiwa zawadi zao kwa wakati na kuwashukur wadhamini Azam TV kwa kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum.

Naye Makamu wa Pili wa Taff, Rahel Pallangyo alizishukuru klabu zote zilizoshiriki pamoja na Azam TV kwa kudhamini mashindano hayo huku akiomba wadhamini zaidi kwa sababu watu wenye ulemavu nao wana haki ya kushiriki michezo.

Mashindano hayo ambayo yalifanyika kwa siku tatu yalishirikisha timu za Ubungo, Sauti Parasports na Pugu Para za Dar es Salaam, Magharibi A ya Unguja na Arusha Warriors na Black Eagle za Arusha, Songwe, na Wilaya ya Mjini ya Zanzibar.


 

Post a Comment

0 Comments