DKT.SAMIA SULUHU HASSAN ASISITIZA WAANDISHI WA HABARI KUZINGATIA WA TAKWIMU KWENYE KALAMU ZAO


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuzingatia matumizi ya takwimu sahihi wanapoandaa na kuwasilisha taarifa kwa umma, akisema uandishi wa habari unaojikita kwenye takwimu una faida kubwa kwa jamii na huonesha kwa uwazi maendeleo yanayofanywa na Serikali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 5 Mei 2025 katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Samia Kalamu Awards, Rais Samia alisema uandishi wa habari unaotumia takwimu si tu kwamba unaongeza weledi katika tasnia, bali pia unasaidia kujenga uelewa wa kina kwa wananchi kuhusu hali halisi ya mambo.

Rais Samia pia aliwahimiza waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla, kuendelea kutumia uhuru walionao katika kuhabarisha jamii kwa weledi na uwazi, lakini wakizingatia pia uzalendo kwa taifa. Alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kulinda na kukuza uhuru wa vyombo vya habari, lakini ni jukumu la wanahabari kuhakikisha wanatumia uhuru huo kwa manufaa ya taifa.

Vilevile, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha sanifu ya Kiswahili katika vyombo vya habari, akieleza kuwa lugha hiyo ni chombo muhimu cha mawasiliano na maendeleo, na matumizi yake sahihi yatachangia kukuza na kuendeleza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Hafla hiyo ya tuzo iliandaliwa kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa waandishi wa habari waliobobea katika uandishi bora, wenye kuzingatia maadili, ukweli na maslahi ya taifa.

Post a Comment

0 Comments