RC DANIEL CHONGOLO ARIDHISHWA NA UJENZI WA BWALO LA CHAKULA SHULE YA DR SAMIA SULUHU HASSAN

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe.Daniel Chongolo, ameshindwa kuzuia hisia zake na kutamka kwa msisitizo kuwa  “ mmefuta hasira zangu” baada ya kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Kata  ya Namole Halmashauri ya Mji Tunduma Wilayani Momba.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo uliokuwa na changamoto za utekelezaji katika hatua za awali RC Chongolo amesema sasa ameridhika na kazi nzuri ya usimamizi na utekelezaji unaoendelea.

"Nakupongeza sana Mkuu wa Wilaya na uongozi wa Halmashauri  leo mmefuta hasira zangu zote kwani  nimeona na kufurahishwa na kazi nzuri ya usimamizi mliyoifanya katika mradi huu" amesema Chongolo. 

"Mara ya mwisho nilipokuja hapa nilikataa hata kusaini kitabu cha wageni lakini sasa mmefuta hasira zangu” amesema Chongolo.

Bwalo hilo la chakula ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu takribani Mil. 800 awali utekelezaji wake ulianza kwa kusuasua jambo lililomkera RC Chongolo. 

Mhe. Chongolo amefanya ziara ya siku moja ya kutembelea Halmashauri hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Halmashauri zazMkoa kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tunduma Mariamu Chaurembo  amesema tayari Halmashauri imefanya mabadiliko ya bajeti na kutenga kiasi cha Mil  350 kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki.
 Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa ameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha ifikapo Aprili 25 mwaka huu bwalo hilo linaanza kutumika rasmi na ameahidi kushiriki chakula cha pamoja na wanafunzi kama ishara ya mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo.

Post a Comment

0 Comments