FATHER JOHN MTWALE ATOA WITO VIONGOZI WA DINI KUJIENDELEZA KIELIMU


Father John Mtwale  kutoka Jimbo Katoliki la Mwanza amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi wa dini kujiendeleza  kupata elimu mara kwa mara ili kuweza kupanua wigo wa uongozi kwa waumini wa dini wanao waongoza katika jamii.

Father Mtwale amesema hayo mara baada ya kuhitimu mafunzo ya siku tano  ambapo yeye ni miongoni mwa wahitimu 21 wa mafunzo ya uongozi  katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu  Julius Nyerere  iliyopo Kwa Mfipa Kibaha Mkoani Pwani. 

Father Mtwale amesema kuwa ana imani kubwa kuwa yeye na wahitimu wengine  wataenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata katika sehemu zao wanazoziwakilisha.

"Mafunzo haya yametuongezea ufahamu wa uongozi na yametufungua na ufahamu wa Mambo mbalimbali na kutupatia mbinu kama viongozi za kutawala hisia pindi tunapokuwa na ghadhabu kama binadamu  katika  kutoa maamuzi sahihi"  amesema  Father Mtwale.

"Natoa wito kwa   viongozi wa dini zote pindi watakapopata fursa waje hapa ii wajiendeleze hapa shuleni  na matunda yake  watayaona" amesema  Mtwale .

Aidha Father Mtwale  amesisitiza  viongozi wa dini wote wajitokeze kwenda kupata  mafunzo haya yapo hayana mipaka yanasaidia kuibadilisha jamii nzima viongozi wote tuungane katika kuleta mabadiliko ya kweli na siyo kwa viongozi wa dini pekee.

"tumejifunza namna ya kutawala hisia na kuwa watulivu hivi sasa  dunia imekumbwa na  matatizo ya kupata mfadhaiko na sonona changamoto hii  imekithiri duniani kote,hivyo ukiwa kiongozi changamoto zipo ila ufundi wa kiongozi ni kuzivuka na kuzikabili changamoto hizo" amesema Father Mtwale.

Wakati huohuo Mkuu wa  Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda amewataka Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali nchini kutumia Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kuwapa mafunzo na elimu ya Uongozi ya uwajibikaji watumishi wao ili kuondokana na changamoto za migogoro kazini.

Akizungumza mara baada ya kufunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi kutoka Taasisi mbalimbali hapa nchini katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwa Mfipa Kibaha  Mkoani Pwani hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda akiwa Mgeni Rasmi amesema shule hiyo ina miundo mbinu bora na elimu inayotolewa ni msaada mkubwa kwa watumishi na wafanyakazi nchini.

Amesema kuna changamoto baina ya wafanyakazi hutokea kwasababu ya matatizo yanayotokana na ukosefu elimu ya uongozi ya uwajibikaji kazini hivyo wanapopata mafunzo hayo kila mmoja hujitambua na migogoro kazini inakwisha.

"Kwa zile Taasisi za Halmashauri na Wilaya zote nchini kada za waalimu waalimu wa taaluma na maadili wote nawashauri waje wapate elimu ya mafunzo ya uongozi katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ili waweze kuongeza wigo wa elimu zao hata kama tayari wako maofisini kwani elimu haina mwisho" amesema Mapunda.

Amesema kuwa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere ziba ombwe la changamoto elimu ya uongozi kwa viongozi kazini katika nyanja za kada zote nchini hivyo taasisi na idara mbalimbali za serikali na binafsi zitumie kuendeleza watumishi wao.

 Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere John Baytani amesema mafunzo hayo kwa viongozi hao yametolewa kwa kuzingatia ubora pia wamejifunza mambo mbalimbali ikiwamo afya ya akili na namna ya kuongoza rasilimali watu ambapo wametoka wakiwa wameiva.

Baytani amesema wahitimu hao 21 ambao wamepatiwa mafunzo ya uongozi ni vijana kutoka Taasisi mbalimbali nchini na mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wengine kuona namna ya kujipanga kwenda kujifunza na kupata elimu hiyo ya uongozi shuleni hapo.

Post a Comment

0 Comments