Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kwamba Mwijaku aliyetajwa katika video ya mabinti wanafunzi wa vyuo vikuu waliomdhalilisha binti mwenzao, atahojiwa.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo Aprili 23, 2025, Dkt. Gwajima amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria kuhusu kuwahoji wahusika wa tukio hilo. “Aidha, kwa upande mwingine, jamii nayo imeendelea kuhoji mbona aliyetajwa kuwa ni Mwijaku hakamatwi?.”
Waziri Gwajima amewahakikishia wananchi kuwa, Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hao, naye atahojiwa kwa mujibu wa Sheria na baada ya hapo, Wizara yake itaona nini ifanye kuhusu mustakabali mzima wa maadili ya jamii na nafasi ya huyo Mwijaku na wengine wote wenye nafasi zenye kuchochea kasi ya athari chanya au hasi kwenye maadili ya jamii.
Waziri Gwajima pia, amewaomba wananchi wawe watulivu na kuongeza kuwa waendelee kufuatilia taarifa za Jeshi la Polisi.
Katika video hiyo iliyoanza kusambaa usiku wa kuamkia Aprili 20, 2025 inaonekana msichana ambaye jina lake bado halijatambulika akidhalilishwa, kupigwa na wahusika wanaodaiwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku wakimtaja mhusika kwa jina moja la Mwijaku.
Tayari UDSM na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wamekwisha kutoa taarifa za kulaani tukio hilo.

0 Comments