RAIS MWINYI:UNESCO ISAIDIENI ZANZIBAR KATIKA UCHUMI WA BULUU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amelishauri Shirika la Elimu , Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuisaidia Zanzibar kuendeleza Uchumi wa Buluu kwani ni sekta muhimu kwa Uchumi na Ustawi wa wananchi wake.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipozungumza na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu  Audrey Azoulay  waliofika Ikulu Zanzibar tarehe 5 Machi 2025.

Aidha Rais Dkt. Mwinyi ameuelezea Ujumbe huo kuwa  kwa sasa sekta ya Uchumi wa buluu ndio kipaumbele cha Serikali inayohitaji  kupewa msukumo wa ziada wa misaada ya kitaalamu,Teknolojia na fedha ili kuwa endelevu na kuiwezesha nchi kunufaika na Rasilimali za kutosha ziliomo baharini.

Amefahamisha kuwa Uchumi wa buluu una fursa nyingi zinazoweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo  na ukuaji wa Uchumi, fursa za ajira na kuimarisha maisha ya wananchi na kuishauri UNESCO kuwa tayari kushirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo.

Rais Dkt.Mwinyi  amesema bado zipo changamoto nyingi katika kuuendeleza mji mkongwe ili ubaki katika haiba na urithi wake kutokana na kuwa na idadi kubwa ya nyumba zinazohitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, Udhibiti wa Uingiaji na utokaji wa Magari unaopaswa kubadilika kulingana na Mazingira ya sasa ndani ya Mji Mkongwe bila kuathiri Maisha ya wakaazi wa Mji huo.

 Naye, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay ameihakikishia  Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo katika juhudi za kuleta Maendeleo endelevu  katika sekta tofauti na ustawi wa watu wake na kusisitiza kuwa shirika hilo liko tayari kuchukua juhudi maalum  na misaada  ya kitaalamu ,teknolojia na Uzoefu kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu na kupongeza Mafanikio yaliofikiwa katika sekta ya elimu hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments