Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeanzisha huduma ya kinamama wajawazito kujifungulia katika jakuzi maalum (water birth).
Huduma hiyo ambayo itapatikana kwa sh 1,500,000 sawa na kuweka sh 166,666.6666666666 kila mwezi kwa miezi tisa imeelezwa kuwa bora na yenye kumsaidia mama kupunguza uchungu na kumuepusha kuchanika wakati wa kujifungua.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Dkt. Debora Bukuku amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa hospitali hiyo kupanua wigo wa huduma.
Hapo awali katika Hospitali zote za Umma huduma hizo zilikuwa zinapatikana Muhimbili Upanga pekee .
Kwa upande wake Muuguzi Mkunga Bingwa na Mtaalam wa kusaidia kinamama kujifungulia kwenye jakuzi Bw. Rwehabura France amesema miongoni mwa faida za mama kujifungulia kwenye jakuzi ni pamoja kupata fursa ya kukaa na wataalam na ndugu atayemchagua kukaa naye kwa muda wote atakaokuwa kwenye jakuzi kitu ambacho kitamuongezea faraja zaidi na kutohisi maumivu.
Bw. France ameongeza kuwa kabla ya mama kupatiwa huduma hiyo huwa anapatiwa elimu kuhusu mtiririko wa huduma hiyo ambapo pia amebainisha kuwa huduma hiyo ni salama kwa mama na mtoto atakayezaliwa.
Kwa upande mama aliyejifungulia kwenye jakuzi hospitalini hapo Bi. Rahel Mushi amesema amefurahishwa na huduma hiyo kwa kuwa wataalam walikuwa wanampatia mazoezi wakati wote akiwa kwenye jakuzi na kumfanya asihisi maumivu, hivyo anawashauri wakina mama wengine kutumia huduma hiyo.
0 Comments