NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AITAKA NCAA KUSIMAMIA KAZI ILIYOASISIWA NA RAIS KIKAMILIF


Na mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kusimamia kikamilifu shughuli za utalii ili kulinda kazi iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza sekta hiyo kimataifa na kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema kwamba katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuwa kivutio bora duniani ni vema ikaongeza nguvu katika kuboresha miundo mbinu ya barabara ambapo itasaidia kuimarisha shughuli za utalii na kuongeza idadi ya watalii.

“Kazi kubwa ya kutangaza utalii imefanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo ni jukumu letu kusimamia kazi hiyo na tusikubali kurudi nyuma,imarisheni miundo mbinu ya utalii ili nchi yetu iendelee kuwa na sifa kubwa kimataifa”, alisema Naibu Waziri  Kitandula.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye alimhakikishia Naibu Waziri Kitandula kwamba Mamlaka itayafanyia kazi maelekezo yote ili kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua na hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Mheshimiwa Kitandula ametoa kauli hiyo mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili mwishoni mwa wiki aliyoifanya ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kukagua miundo mbinu ya barabara na kuzungumza na menejimenti ya Mamlaka hiyo ikiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Dkt. Elirehema Doriye.
Katika ziara yake hiyo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dunstan Kitandula alitembelea  barabara ya Loduare mpaka Golini kuelekea Serengeti, Barabara ya Ndutu kuelekea Endulen,Barabara ya Olduvai kupitia Golini na alipata nafasi pia ya kukagua ujenzi wa jengo la makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lililopo pembezoni mwa mji wa Karatu.

Post a Comment

0 Comments