Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Edson Mwakihaba amewataka madereva wa vyombo vya moto kuheshimu alama na michoro ya barabarani wanapoendesha vyombo hivyo ili kuepusha ajali.
Amezungumza hayo Leo Septemba 21,2024 katika Maadhimisho ya miaka 10 ya mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) ambapo alitoa elimu kwa madereva wa mabasi na pikipiki katika kijiwe cha Njuweni na kituo kikuu cha mabasi ya Mkoani, Wilayani Kibaha kuhusu utii wa sheria za usalama barabarani.
Mwakihaba amesema kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Pwani hawatosita kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wote ambao watabainika kuvunja Sheria hizo kwa makusudi.
Aidha, amewapongeza mabalozi wa Usalama barabarani kwa utoaji wa elimu na kusaidia utoaji wa taarifa za madereva wanaokiuka sheria kwa makusudi na kupelekea kupungua kwa ajali katika Mkoa wa Pwani.
Kadhalika, Mwakihaba amewataka madereva wa mabasi kuwa mfano na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale wanapoona kuna madereva wengine wanaendesha gari kwa mwendo hatarishi ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati badala ya kusubiri kupiga simu pale barabara inapokuwa imefunga tu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mabalozi wa usalama barabarani Kanda ya Mashariki,Godfrey Mali ametoa wito kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kuacha kutumia vinywaji mbalimbali vya kuongeza nguvu na kuchanganya na dawa mbalimbali kama panadol na flagili ili kuondoa uchovu, Ameeleza kuwa uchovu dawa yake ni kupumzika na si vinginevyo.
Aidha, Mali amewataka madereva hao kuzingatia matumizi ya kofia ngumu kwao na kwa abiria wanaowapakia pamoja na kuacha kupakia abiria zaidi ya mmoja jambo ambalo ni hatari sana endapo ikitokea ajali.
0 Comments