UWEKEZAJI WAONGEZEKA KATIKA SEKTA YA UTALII NCHINI

Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kumekuwa na ongezeka la uwekezaji katika miundombinu na mahitaji yanayochangia ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini.

Hayo yamesemwa  jana Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii  Ramo Makani wakati akijibu Hoja mbalimbali za Wabunge .

“Kumekuwa na Ongezeko la uwekezaji katika ujenzi wa Hoteli na Madaraja mbalimbali,uimarishaji wa vyombo vya usafiri kuelekea ndani ya Hifadhi na Maeneo mengine yenye vivutio na uboreshaji wa vifaa mbalimbali vinavyotumika kuhudumia watalii,mambo ambayo kwa kiwango kikubwa hutekelezwa na Sekta binafsi “Aliongeza Mhe.Makani.

Aidha amesema mafanikio hayo yamewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii ambapo mwaka 2016 idadi hiyo iliongezeka kutoka jumla ya Watalii milioni 1,137,182 kwa mwaka 2015 hadi jumla ya watalii 1,284,279 kwa mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 12.9 ambapo ongezeko hilo limeonekana katika Hifadhi za Taifa zinazosimamiwa na TANAPA.

Ameongeza kuwa ili ongezeko ili liwe na tija na endelevu Wizara hiyo imejikita katika kusimamia ubora wa huduma na utoaji huduma,kutangaza zaidi vivutio hususani vivutio vipya na kusambaza shughuli za Utalii nchi nzima hususani ukanda wa kusini.

“Kwa upande wa Serikali ujenzi wa barabara na viwanja vya Ndege,Ununuzi wa ndege mbili na zingine nne zinatarajiwa kuja katika siku za karibuni izi zote ni jitihada zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Utalii nchini”alisisitiza Makani.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa Sekta Binafsi kuongeza mbinu,bidii na mitaji kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza Utalii na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments