Hatua hiyo inakuja ikiwa, Sera ya Taifa ya Utalii iliyopo ilifanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 17 iliyopita.
Katika kutambua hilo, Wizara imeanza kupitia upya Sera hiyo ili kuhakikisha Sekta ya Utalii inakwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani yakiwamo ya teknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira akizungumza katika mkutano unaofanyika kwa muda wa siku mbili Jijini Arusha kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki alisema Sera inafanyiwa marekebisho kwa kuwa imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika sekta hiyo.
Aidha, alisema kwa kutambua mchango wa utalii kiuchumi , ni wazi kuwa sera wezeshi ya utalii yenye kutoa mwongozo wa utaratibu bora na sahihi wa usimamizi, uendelezaji na utendaji katika sekta hiyo unahitajika.
’’ Tunataka kuibadilisha sera hiyo ili iweze kujibu changamoto za aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo, akitolea mfano utalii mikutano pamoja na utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini. Kutokana na hali hiyo, Dkt. Nzuki amesema marekebisho ya Sera hiyo yanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wadau kwa kuwa inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na Sekta Binafsi katika kutoa huduma na kufanya biashara za utalii hapa nchini.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga alisema uhuishwaji wa Sera hiyo utazingatia namna ambavyo wazawa wataweza kuwa wanufaika namba moja kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya kuendesha biashara ya utalii tofauti na sasa ambapo makampuni mengi ya utalii ni ya watu kutoka nje.
Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Richard Lugimbana alisema sera iliyopo sio mbaya ila tatizo lililopo Serikali imeshindwa kuitekeleza licha ya kuwa kuna baadhi ya vitu muhimu ambavyo havimo kwenye sera hiyo ikiwemo changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Aliongeza kuwa mara baada ya kuhuisha sera hiyo itaweza kusaidia kuonesha jinsi gani wadau wa utalii wanayokumbana na changamoto mbalimbali katika kuwahudumia watalii. Kwa upandwe wa Mwenyekiti wa TATO, Wilbert Chambulo alisema suala la kuifanyia marekebisho ya sera hiyo ni jambo jema ila sasa serikali iangalie namna ya kuboresha mashirikiano katika utoaji wa maamuzi kwa wafanyabiashara wa utalii nchini badala ya kuamua yenyewe pekee yake Mkutano huo wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau umeanza kufanyika Mkoani Arusha kwa kuwashirikisha wadau kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini na badaaye utafanyika katika kanda zingine kwa muda wa siku mbili mbili kwa ushirikiano kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirikisho la Vyama Vya Utalii Tanzania (TCT) pamoja na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu .
0 Comments