WADAU WAOM A MIUNDOMBINU STENDI YA MABASI MBAGALA

 Kijana akisukuma tolori huku akipita kwenye matope katika Stendi ya mabasi ya Mbagala Rangitatu jijini Dar es Salaam jana. Watumiaji wa stendi hiyo wameomba Manispaa ya Temeke kuwawekea miundombinu mizuri ili kuruhusu maji kupita katika kipindi hiki cha mvua.
 Muonekano wa stendi hiyo katika kipindi hiki cha mvua.
Wafanyabiashara wakiendelea na biashara zao kwenye stendi hiyo.

Na Dotto Mwaibale

WATUMIAJI wa Stendi ya Mabasi ya Mbagala Rangitatu jijini Dar es Salaam wameiomba Manispaa ya Temeke kuboresha miundombinu ya stendi hiyo katika kipindi hiki cha mvua ili kuondoa adha wanayokabiliana nayo ya kujaa maji.

Ombi hilo limetolewa Dar es Salaam jana na wafanyabiashara na madereva wanaotumia stendi hiyo wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto hiyo waliyonayo ya kujaa maji hasa katika kipndi hiki cha mvua za masika.

Mfanyabiashara ndogo ndogo katika stendi hiyo,  Afidh Abdallah alisema katika kipindi hiki cha mvua stendi hiyo imekuwa ikijaa maji na kusababisha matope hivyo kuwa kero kwao.

"Mvua ikinyesha hatuwezi kufanya biashara katika stendi hii tunashindwa kuzunguka kufuata wateja" alisema Abdallah.

Abdallah alisema kwa kutumia fedha wanazolipa ushuru kila siku manispaa hiyo inaweza kuwawekea hata molamu kwa kipindi hiki cha mvua ili kupunguza madimbwi ya maji wakati wakisubiri kujenga miundombinu ya kudumu.

Mama Lishe katika stendi hiyo Mwajabu Mohamed alisema maji yanapo jaa katika stendi hiyo wateja wao wamekuwa wakishindwa kufika kupata chakula kutoka maeneo mengine kwa kuhofia madimbwi na matope yanayokuwepo.

Said Khatibu ambaye ni dereva wa basi la Manshallah linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini alisema wakati huu wa mvua changamoto kubwa inayokuwepo eneo hilo ni kushindwa kupata nafasi ya kupakia na kushusha abiria kutokana na maji yanayojaa.



Post a Comment

0 Comments