Mwandishi wa vitabu Ritha Tarimo akiongea na wageni waalikwa wakati wa uzinduzi wa kitabu chake cha 'Colour of Life'. |
(PICHA/HABARI NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe amewataka vijana kutumia muda wao kujenga utamaduni wa
kujisomea vitabu badala ya kupoteza muda wao mwingi katika mitandao ya kijamii
kwakuwa kusoma vitabu ndiyo msingi mzuri wa elimu.
Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa
akizindua Kitabu cha “Colour of Life” kilichoandikwa na Mwandishi Ritha
Tarimo ambapo katika hotuba yake
aliyoitoa mbele ya wageni waalikwa amesisitiza suala la vijana kujenga
utamaduni wa kupenda kusoma vitabu ili kukuza elimu yao.
Mhe. Mwakyembe ameeleza kuwa, baadhi ya vijana siku hizi wamekuwa
wakitumia muda wao mwingi katika mitandao ya kijamii badala ya kujisomea, hivyo
amewashauri wajifunze kutoka kwa Mwandishi wa Kitabu hicho ili waje kuwa
waandishi hodari wa kutegemewa na Taifa.
Sambamba na rai hiyo, Waziri Mwakyembe amempongeza Ritha
Tarimo kwa juhudi zake kubwa na maarifa katika kutunga na kuandika kitabu hicho
ambacho amesema kuwa kitabu hicho ni kizuri na kina maudhui mazuri kwa vijana
hususani wanafunzi, hivyo ameitaka jamii kumuunga mkono kwa kukisoma ili jamii
ipate kuelimika.
“Ukimkuta mtu kama Ritha Tarimo anaandika kitabu katika
kipindi hiki ambapo vitabu vinaonekana kuondolewa kwasababu ya maendeleo ya
teknolojia, ni vema kumpa moyo na kumuunga mkono kwakuwa yeye ametuonyesha
Watanzania kuwa hata sisi tunaweza, na kitabu hiki niwaambie ukweli kina
maudhui ya kumtia moyo kijana ya kutokata tamaa katika maisha”, alisema Dkt.
Mwakyembe.
Ameongeza kuwa, Serikali inauunga mkono juhudi zake za
uandishi wa vitabu vyake na amechukua baadhi ya nakala za kitabu hicho kwa
ajili ya kuzipelekeka kwa Waziri husika wa masuala ya Elimu Sayansi na
Teknolojia ili kuona namna gani kitabu hicho kinaweza kuisaidia jamii.
Kwa upande wake Mwandishi Ritha Tarimo ameishukuru Serikali
kwa kukubali wito wa kukizindua kitabu chake na pia utayari wa Serikali katika
kumuunga mkono ili uandishi wake uwe wenye tija kwa jamii ya Watanzania.
Ameeleza kwamba, kazi ya uandishi ameinza muda mrefu na leo
ameweza kupata nafasi ya kuungwa mkono na Serikali pamoja na Watanzania
mbalimbali ikiwemo familia yake na hatimaye kukamilisha kitabu hicho na
kukizindua rasmi.
“Nakushukuru Mhe. Waziri kwa kutumia muda wako kuja
kukizindua kitabu hiki, nakushukuru sana na sasa naamini ndoto zangu zinatimia,
kitabu hiki nimekitengeneza katika umbo dogo ili kiweze kuwavutia watu wengi
kwani kina maudhui mazuri kwa vijana na jamii nzima ya Kitanzania”, alisema
Ritha.
Kitabu cha Colour of Life ni moja kati ya vitabu saba
alivyoandika Mwandishi huyo ambacho pia kimepata fursa ya kuzinduliwa na Waziri
Dkt. Harrison Mwakyembe na kwa mujibu wa mwandishi huyo, kitabu hicho kina
maudhui mazuri kwa vijana katika kuwajenga kimaisha.
0 Comments