TAMTHILIA YA MFALME KIMA YA CHINA ILIYOTAFSIRIWA KWA KISWAHILI YAZINDULIWA

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel (wa nne kutoka kushoto) na Naibu Waziri wa Masuala ya Utangazaji, Filamu na Habari wa China, Tong Gong (katikati), wakikata utepe kuzindua maonyesho ya kwanza ya tamthiliya ya China ya 'Mfalme Kima' iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kushoto ni Jiang Almin, ambaye ni Mkurgenzi wa Radio China Kimataifa, wa pili kutoka kulia ni Suzan Mungy (Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la Utangazaji Tanzania - TBC) na wa nne kulia ni Ma Li (Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa wa China).

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel,  akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya kwanza ya tamthiliya ya China ya 'Mfalme Kima' iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. 
 Ma Li, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa wa China, akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo hii jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Mtendaji wa StarTimes, Guo Zingi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamthiliya ya 'Mfalme Kima' ambayo ni ya Kichina iliyotafsiriwa kwa Kiswahili.
 Suzana Mungy, Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamthiliya ya Kichina ya 'Mfalme Kima' iliyotafsiriwa Kiswahili. Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurgenzi wa Radio China Kimataifa,  Jiang Almin, akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
 Meza kuu ya wageni wa heshima katika uzinduzi huo.
 Akinadada wa StarTimes wakiwa wamejiandaa kabla ya kukatwa kwa utepe kuashiria uzinduzi wa maonyesho ya kwanza ya Tamthiliya ya China ya Mfalme Kima iliyotafsiriwa kwa Lugha ya Kiswahili.
Wageni waalikwa wakifuatilia mambo yaliyokuwa yakiendelea.
 Wasanii wakitumbuiza kwenye uzinduzi huo.
 Wageni mbalimbali wakifuatilia.
Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa StarTimes, wasanii wa wageni wa heshima.

Na Dotto Mwaibale

SERIKALI ya China kupitia Wizara ya Utamaduni ya nchi hiyo imeombwa kutangaza filamu za Tanzania nchini humo ili kuutangaza utamaduni wa Watanzania.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo hii na Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Suzana Mungy, wakati akitoa hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC katika hafla ya uzinduzi wa maonesho ya kwanza ya Tamthiliya ya China ya (Mfalme Kima) ya lugha ya Kiswahili uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam leo.

"Ni vema sasa na wenzetu wa China wakawa wanaonesha filamu zetu huko kwao kwa lugha ya Kichina ili kusaidia kutangaza utamaduni wetu," alisema Mungy.

Mungy alisema Wachina wamekuwa wakionesha filamu zao hapa nchini ambazo zimeingizwa sauti kwa lugha ya Kiswahili na Watanzania hivyo ili kupanua wigo wa mahusiano katika tasnia hiyo ni vema pande zote mbili zishirikiane kuandaa tamthiliya ya pamoja ya lugha ya Kiswahili.

Mkurugenzi Mtendaji wa StarTimes, Guo Zingi, alisema kwamba kampuni yake imejizolea mashabiki wengi nchini Tanzania kutokana na kuonesha filamu na tamthiliya nyingi za Kichina zilizotafsiriwa Kiswahili, lugha ambayo inaeleweka.

Alitolea mfano tamthiliya ya Maudodo, kama mojawapo ya tamthiliya hizo ambayo ilijizolea umaarufu kwa watu wa rika zote nchini Tanzania.

Aidha, amekiri kwamba, kwa sasa ziko tamthiliya na filamu nyingi za Kichina zinazotazamwa nchini Tanzania ambazo zimetafsiriwa Kiswahili.

Alisema mapema mwaka 2016 kampuni hiyo ilifanya mashindano ya kuwapata vijana 10 wa Kitanzania waliopelekwa China kwa lengo la kwenda kuingiza sauti za Kiswahili katika filamu na tamthiliya mbalimbali za Kichina, hatua ambayo imesaidia kuzifanya tamthiliya hizo zipendwe na kukubalika nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Masuala ya Utangazaji, Filamu na Habari wa China, Tong Gong, alisema uhusiano huo baina ya Tanzania na China utaendelea kudumishwa katika masuala ya utamaduni kama iliyo katika maeneo mengine maendeleo.

Kupitia tamthiliya mbalimbali, watakuwa wakibadilisha utamaduni baina ya nchi hizo mbili.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel, alisema Tanzania na China wataendelea kushirikiana na kudumisha uhusiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo - Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tsetung.

"Kwa kuwa wenzetu China mko juu katika teknolojia ya utangazaji na mawasiliano, ninawaomba muangalie namna ya kuisaidia Tanzania katika tasnia ya sanaa na utamaduni ili na wasanii wetu nao kazi zao ziweze kupata masoko huko," alisema Profesa Ole Gabriel.


Post a Comment

0 Comments