SUMATRA WAANZA KAMPENI YA KUTOA ELIMU NJIA HALALI KUSAFIRISHA MAZAO


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeanza kampeni ya kutoa elimu juu ya njia halali za usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mkaa katika barabara kuu zilizopo nchini kote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Tulizo Kilaga alisema uvunaji holela na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu hususan wa mkaa kwa kutumia pikipiki na baiskeli kutoka misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata hifadhi za Taifa, unatajwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.

Hivyo TFS imeamua kutoa elimu kwa umma kabla ya kuchua hatua za kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji kwa lengo la kudhibiti uharibifu huo kabla nchi haijageuka jangwa siku za karibuni.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48 za misitu na misitu mataji wazi ambapo jumla ya hekta 372,000 za misitu huaribiwa kwa mwaka. Kiwango ambacho ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye misitu hapa nchini, na ni sawa na kufyeka zaidi ya hekta 1,000 kwa siku.

Aliongeza kuwa kuwa Jiji la Dar es Salaam peke yake zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa huingizwa katika kipindi cha mwezi mmoja na kuongeza kuwa inakadiriwa pikipiki 20 zikisafirisha mkaa ni sawa na lori moja la tani 7 lililojaa mkaa, na njia hii ya usafiri wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki inakiuka Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu, 2015 unaoeleza kuwa vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirsha mazao ya misitu ni vile vyenye magurudumu manne.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu, Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mossi Ndozero alisema usafiri unaoendelea wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki ni hatarishi na unaokiuka Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002 inayotambua pikipiki na baiskeli kama vyombo vya usafiri kwa ajili ya abiria na si kubeba mizigo.

Aidha, Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi Kavu na Majini, Salum Pazi alisema kwa mujibu wa Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya SUMATRA (Motor cycle and Tricycles), 2010 inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo.

“Kwa sasa tunatoa elimu kwa lengo na baada ya elimu hii watakaokaidi watachukuliwa hivyo ni vema kwa wale wanaofanya biashara za mazao ya misitu husuan mkaa waufate sheria na kanuni za nchi,” alisema Kilaga.

Post a Comment

0 Comments