Na Mwandishi wetu
Serikali yawabwaga wanaopinga Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kutupilia mbali pingamizi hilo.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Wakili wa Serikali Evordy Kyando alisema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali pingamizi lililotolewa na baadhi ya wadau wa habari wakipinga baadhi ya vifungu katika Sheria hiyo baada ya kukosa mashiko.
Alisema kuwa katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017, walalamikaji wanadai kuwa kuna baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza na vinakiuka Ibara ya 18 ya katiba ya nchi.
Aidha, Wakili Kyando alibainisha baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vilivyolalamikiwa ni pamoja na 7 (2) (B) (III) (IV) and (V), 7 (3) (A), (B), (C), (F), (G), (H), (I), (J),8, 9(B), 10(2), 11(4), 13, 14, 19, 20, 21, 24, 25, 26, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54 58 na 59 vya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya 2016.
Akifafanua zaidi, Wakili Kyando alisema kuwa kuna baadhi ya hoja zilizopelekea Shauri hilo kutupiliwa mbali ikiwemo vifungu vya Sheria vilivyolalamikiwa viliandikwa vibaya kulingana na Sheria yenyewe ilivyo, viapo vilivyowasilishwa katika kufungua shauri vilikuwa na makosa, jambo lililolalamikiwa halina mashiko, si la kisheria kutokana na malalamiko ambayo hayaoneshi msingi ulipo ikiwa lengo la Sheria ni kuboresha mazingira mazuri ya waandishi, Elimu, mishaara na vitambulisho.
Jopo la wanasheria linalowakilisha upande wa Serikali liliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Makao Makuu, Mark Mulwambo, Wakili Mwandamizi wa Serikali toka Kanda ya Mwanza Ndamugoba Castus na Wakili wa Serikali Evordy Kyando. Kesi hiyo iliyofunguliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited, wakipinga baadhi ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari 2016.
0 Comments