SERENGETI BOYS WACHANJWA Timu ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys leo Machi 24, wamefanyiwa chanjo ya ugonjwa wa manjano (yellow fever) kabla ya kuanza safari ya kwenda Morocco, Cameroon na Gabon. Timu hiyo imefuzu kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Mei 14 mwaka huu na mapema mwezi ujao itasafiri kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.
Kambi hiyo itakuwa ni ya mwezi mmoja (Aprili 5 hadi Mei 1, 2017) kabla ya kuwa na kambi ya wiki moja huko Cameroon (Mei mosi hadi Mei 7, mwaka huu) na baadaye itafanya kambi nyingine Gabon (Mei 7 mpaka Mei 13) angalau kwa wiki moja kabla ya kuanza fainali hizo Mei 14, mwaka huu.
TFF YAPUNGUZA KIINGILIO MECHI TAIFA STARS
Taifa Stars - timu ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa mwaka 2017 inaingia uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya kalenda ya FIFA.
Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeatangaza kushusha bei ya kiingilio kwa watu watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.
“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio vya bei ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia gharama kidogo kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,” ameagiza Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu watakaoketi Majukwaa Maalumu - VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi VIP “B” na “C” watalipia Sh 10,000. Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake aliwathibitishia Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.
“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu. Kwa upande wa Peter Buffler – Kocha Mkuu wa Botswana, alisema kwamba anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa kikosi cha Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu.
Mchezo ambao pia ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.
MWAMUZI ADONGO AONYWA
Mwamuzi Jacob Adongo amepewa ONYO KALI kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria katika mechi namba 186 kati ya Simba na Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Onyo hilo limetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Kadhalika katika mchezo huo namba 186 (Simba 2 vs Mbeya City 2). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.
Adhabu dhidi ya Mbeya City imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu. Mechi namba 190 (Kagera Sugar 1 vs Majimaji 0). Klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kutokuwa na Daktari kwenye Kikao cha Maandalizi ya Mechi (Pre Match Meeting) na hata uwanjani wakati wa mchezo.
Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Kuu, na adhabu ni uzingativu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu. Pia kwa kutumia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu imefuta kadi ya njano aliyooneshwa mshambuliaji Jaffari Salum wa Mtibwa Sugar katika mechi hiyo namba 175 kati ya African Lyon na Mtibwa Sugar iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kubaini haikuwa sahihi.
Klabu ya Yanga iandikiwe barua ya Onyo Kali kutokana na benchi lake la ufundi kumlalamikia mara kwa mara Mwamuzi wakati wa mechi ya utangulizi ya U20 kati ya timu hiyo na Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kuhusu mechi za Ligi Daraja la Pili (SDL Play Off) Mechi namba 3 (Oljoro 1 vs Transit Camp 1).
Klabu ya Oljoro imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na washabiki wa timu hiyo kumrushia mawe Mwamuzi akiwa uwanjani.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
0 Comments