LEO MACHI 29 NI KUMBUKUMBU YA KIFO CHA TX MOSHI WILLIAM


Marehemu  Shaaban   Mhoja   Kishiwa almaarufu kwa jina la 'TX Moshi' alifariki tarehe 29 Machi mwaka 2006 siku ya  Jumatano  majira ya saa 3 asubuhi na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Keko Machungwa. Jijini Dares Salaam.

Tarehe na siku ya kifo chake vimejirudia mwaka huu na siku hiyo huwa kuna burudani ya Msondo katika ukumbi wa Sugar Ray kwa Sokota maeneo ya  Temeke ,marehemu TX Moshi William alijiunga na Msondo mwaka 1982 akitokea Polisi Jazz.
Miongoni mwa nyimbo alizotunga mara baada ya kujiunga ni pamoja na Ajuza, Asha Mwanaseif, (aliomtungia mkewe), na Ashibaye.

Alitunga nyimbo nyingi lakini nyimbo zilizotia fora sana ni pamoja na Kilio cha Mtu Mzima, Ndoa Ndoano, Piga Ua Talaka Utatoa, Ndoa ya Isihaka Kibene, Kaza Moyo na Ajali.
Wimbo wa Ajali aliutunga baada ya kupata ajali ya kuparamia mti wa mvinje pale Mivinjeni Desemba 16, 2005 iliyompelekea kuvunjika mguu.

TX Moshi William alikua chakaramu na mbunifu wa kutunga vionjo ikiwemo mtindo ujulikanao kama Mambo hadharani na katika nyimbo alipenda kuchombeza vionjo vyenye kutoa raha na kunogesha wimbo mfano utasikia "we nani", " kidogo tu..kidogo tu", "kwanini lakini", " watoto wanachezea umeme", "dispilin", " fair play" nk Wakati wa uhai wake TX Moshi William alipitia katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi ambazo ni pamoja na Safari Trippers, Juwata Jazz.

UDA Jazz, na Polisi Jazz bendi ambayo alitokea wakati anajiunga msondo.
TX Moshi William alijariwa kupata tuzo mbalimbali mfululizo za muziki kama Kilimanjaro Music Award.

Marehemu Moshi alibatizwa jina la TX, na mtangazaji mashuhuri na wa siku nyingi aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania, marehemu Julius Nyaisanga   aliyefahamika kama Uncle J. Nyaisanga alimbatiza jina hilo kutokana na tunzi zake za uhakika.
Nyaisanga alikua mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam  badaye akahamia vituo vya utangazaji vya ITV Radio One na Abood TV.

TX Moshi  William  alizaliwa mwaka 1958  Wilayani Korogwe Mkoani Tanga.
Msanii huyo  TX Moshi William ameacha pengo na kumbukumbu isiyosahaulika kwa wapenzi wa Msondo na ulimwengu wa muziki wa dansi nchini .

Post a Comment

0 Comments