Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lenye dhamana ya kufufua, kukuza na kuendeleza sekta ya Sanaa nchini litatoa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya sanaa siku ya Jumatatu tarehe 27/03/2017 saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984, mojawapo ya majukumu makuu ya Baraza ni kufufua na kukuza shughuli za uzalishaji wa sanaa, ili kukamilisha adhama hii Baraza limeamua kufufua programu yake ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambao wanashika nafasi za juu kitaifa katika masomo ya sanaa husasan Sanaa za Ufundi, Maonyesho na Muziki. Sanaa ni chanzo cha ajira kwa vijana wengi ambao wameweza kujipatia kipato na umaarufu kupitia fani hizi za sanaa.
Hata hivyo masomo haya yamekuwa hayapatiwi kipaumble kama ilivyo masomo mengine katika shule za Msingi na Sekondari.
Tuzo hizi zitakuwa nyenzo kwa ajili ya kujenga hamasa, ari, ubunifu na juhudi katika kuleta maendeleo kupitia masomo ya sanaa. Katika program hii wanafunzi kutoka shule 5 za sekondari zitakazohusika katika kupewa tuzo hizo, shule hizi ni Loyola, Azania za Dar es Salaam, Bukoba ya Mkoa wa Kagera, Darajani toka Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha Sekondari toka mkoa wa Arusha.
Matarajio ya BASATA kuwa utoaji wa tuzo hizi utachochea wanafunzi wengi kusoma masomo ya sanaa, kuongeza ubunifu katika kazi za Sanaa na kuwasaidia katika kuongeza ufaulu wao darasani hasa ikizingatiwa Sanaa ni nyenzo katika kumuandaa mtoto kielimu na kimaadili.
Itakumbukwa kuwa BASATA limekuwa na mwendelezo wa programu mbalimbali za Sanaa kwa watoto zilizoanza tangu miaka ya 1980 ambazo zimepata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii. BASATA linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa kufika kwa wingi kushuhudia utoaji wa tuzo hizi.
Sanaa ni kazi, tuipende, tuikuze na kuithamini
Godfrey Mngereza KATIBU MTENDAJI
0 Comments