Immaculate Makilika -MAELEZO
Wabunge nchini Rwanda wamepitisha kwa kauli moja muswada wa sheria ya kuifanya lugha Kiswahili kuwa lugha rasmi nchini humo.
Kufuatia hatua hiyo, sasa Kiswahili nchini Rwanda kinakuwa moja kati ya lugha tatu za Kinyarwanda, kiingereza na kifaransa zinazozungumzwa na wananchi kama lugha rasmi miongozi mwao na kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya nne nchini humo.
Lugha ya Kiswahili nchini Rwanda inatazamiwa kuanza kutumika katika shughuli za uongozi na katika nyaraka za kiofisi.
Aidha, Waziri wa Michezo na Utamaduni nchini Rwanda, Julienne Uwaci alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na lugha hiyo kuwa na wazungumzaji wengi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo kuweza kurahisisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Aliongeza kuwa, “Kiswahili ni lugha rasmi ambayo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatakiwa kuitumia kwa kuwa kitaongeza tija kwa nchi ya Rwanda kufaidi matunda ya utengano wa kiuchumi” Wabunge mbalimbali wa nchi hiyo wametoa maoni, akiwemo mbunge Jean Baptiste Rucibigango ambapo alisema kuwa “Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na watu wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki na hakika itakuwa na faida kuzungumzwa nchini Rwanda”.
Kiswahili kuwa lugha rasmi katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, kunaleta faida nyingi ikiwemo kuongeza wigo wa shughuli za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi wananchama ambazo ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Sudani ya Kusini, pamoja na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizi.
Hatua hiyo ya Rwanda kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya rasmi ya Taifa ni fursa ya adhimu kwa nchi jirani zinazozungumza zaidi Kiswahili ikiwemo Tanzania, kwani itasaidia raia wake kuwa na nafasi murua kushiriki katika shughuli za kibiashara na elimu.
0 Comments