Mwenyekiti wa Umoja wa Jamii
ya watu kutoka India, Bengali waliopo Tanzania (Bango Sangho), Kunal
Banerjee akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kambi ya
upimaji afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano inayotayotaraji
kufanyika katika Shule ya Msingi Kibugumu iliyopo Kigamboni jijini Dar
es Salaam. Katikati ni Mmoja wa madaktari watakaoendesha zoezi la
upimaji afya kwa watoto hao Dkt. Ali Mzige kutoka Kliniki ya Al Hilal ya
jijini Dar es Salaam.
Umoja wa Watu kutoka Bengali,
India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) unataraji kutoa huduma ya
upimaji wa afya bure kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano,
upimaji utakaofanyika Jumapili ya Machi, 13 katika Shule ya Msingi
Kibugumu iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Akizungumzia huduma hiyo,
Mwenyekiti wa Bango Sangho, Kunal Banerjee amesema huduma hiyo
itawawezesha wazazi kutambua magonjwa yanayowakabili watoto wao bila
kulipa malipo yoyote kwa kutambua umuhimu wa afya ya watoto kwa
maendeleo ya taifa.
Alisema kupitia huduma hiyo
madaktari watawapima watoto walio na umri chini ya miaka mitano afya ya
kinywa, uzito, ukaguzi na ushauri wa lishe hivyo kuwataka wazazi
kuwapeleka watoto wao ili waweze kupata huduma bure.
Mmoja wa madaktari
watakaoendesha zoezi la upimaji afya kwa watoto hao Dkt. Ali Mzige
kutoka Kliniki ya Al Hilal ya jijini Dar es Salaam akifafanua jambo
kuhusiana na umuhimu wa kupima afya za watoto katika mkutano na
waandishi wa habari.
“Tunataka kusaidia marafiki zetu
wa Tanzania na katika kuendelea hilo tutatoa huduma ya bure kwa watoto
kupima afya zao na tunataka wazazi wawalete watoto ili wapime afya,”
alisema Banerjee.
Nae Dkt. Ali Mzige kutoka Kliniki
Al Hilal alisema Bango Sangho kimekuwa chama ambacho kikisaidia jamii ya
Tanzania katika sekta ya afya na wamekuwa wakitoa huduma ya kupima
watoto bure walio na umri chini ya miaka mitano kwa mwaka wa tatu
mfululizo.
Alisema ripoti ya afya Tanzania
inaonyesha kuwa kuna watoto 81 wamekuwa wakipoteza maisha kati ya watoto
1,000 walio na umri chini ya miaka mitano kutokana na sababu mbalimbali
ambapo wamekuwa hawapati huduma na kupitia huduma hiyo ya kuwapima bure
watoto walio na magonjwa wataweza kutambulika.
“Tutafanya huduma ya kupima bure
watoto walio chini ya miaka mitano na tutakaobaini wanamatatizo maalum
ya kiafya tutawapa rufaa ili wakapate huduma ya matibabu,” alisema Dkt.
Mzige.
Huduma hiyo ya kupima watoto walio
na umri chini ya miaka mitano ilifanyika pia mwaka jana na watoto 289
walipimwa afya zao huku baadhi walikutwa na matatizo ikiwemo maambukizi
ya mfumo wa njia ya mkojo UTI, Utapiamlo, kukatwa vimeo na wengine
wakionekana kuwa na afya duni.
Mtaalamu wa afya ya uzazi
kutoka Kliniki ya Al Hilal, Bi. Husna Abdallah akitoa msisitizo kwa
akina mama kuzingatia kanuni za afya ya uzazi wakati wa mkutano na
waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari wa gazeti
la Tanzania Daima, Zawadi Chogongwe (kulia) akiuliza swali kwa wataalamu
wa afya wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na kambi ya
upimaji afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano inayotayotaraji
kufanyika katika Shule ya Msingi Kibugumu iliyopo Kigamboni jijini Dar
es Salaam.
0 Comments