XIE YI (kulia) akiwa na mdoli wake jijini Beijing, Xie Yi aliamua kujiita Hamisi (jina la kiswahili) |
NA KHADIJA KALILI, ALIYEKUWA CHINA
ZIMEKUWAPO juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali
kupitia idara na taasisi zake kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha
lugha adhimu ya Kiswahili ambayo ni moja ya alama ya Mtanzania, inakuwa moja ya
lugha kubwa duniani.
Moja ya matunda ya juhudi hizo ni kuona Kiswahili
kinatumika hata kwa baadhi ya mikutano na makongamano barani Afrika ikiwamo
katika mikutano ya Umoja wa Afrika (AU).
Aidha, nchi nyingi hasa za Ulaya kama Uingereza,
Ujerumani, Ufaransa na nyingine kadhaa, zimekuwa na programu zinazoendeshwa kwa
lugha ya Kiswahili katika redio zao kama BBC Swahili na Deustchwelle (DW) ya
Ujerumani.
Vituo hivi na vinginevyo kama Radio France International
(RFI) ya Ufaransa, wamechangia kwa kiasi kikubwa kukitangaza Kiswahili sio tu
katika nchi zao, pia ndani na nje ya Afrika.
Nikiwa katika ziara ya mafunzo nchini China hivi
karibuni, nilijionea namna lugha hiyo ya Kiswahili inavyotumika na baadhi ya
watu wan chi hiyo licha ya kukumbana na vikwazo kadha wa kadha.
Kwa mujibu wa Msaidizi Mkuu wa Idhaa ya Kimataifa ya
Radio China International (CRI ) Xie Yi, ambaye
pia ni mtangazaji wa kituo hicho anayefahamika zaidi kwa jina la ‘Hamisi,’ lugha
hiyo imekuwa ikipendwa na wengi.
Katika ziara hiyo maalumu ya wanahabari kwenye kituo
hicho, Xie anasema kujifunza Kiswahili si kazi rahisi licha ya wananchi wengi
wa China wangependa waifahamu kutokana na kuzalisha maneno mapya kila kukicha.
Mwandishi wa makala hii akiwa na wengine katika ziara
maalumu ya kimafunzo iliyoratibiwa na Baraza la Habari Tanzania na kudhaminiwa
na Ubalozi wa China nchini Tanzania, walijionea baadhi ya Wachina wakiizungumza
lugha hiyo.
“Wengi wanapenda kujifunza lugha ya Kiswahili, lakini
si kazi rahisi kama wengi wanavyodhani kwa sababu kila kukicha inaleta neno
jipya,” anasema Xie.
Anasema, baada ya serikali ya China kulijua hilo ndipo
wakaamua kuanzisha vyuo vikuu viwili katika mji mkuu wa Beijing ili
kutoa mafunzo ya lugha hiyo huku walengwa wakubwa wakiwa ni wanafunzi waliopata
alama za juu katika mitihani.
“Idhaa hii ya Kiswahili katika Radio China
ilianzishwa 1993, ambapo ilitoa ajira kwa watangazaji kutoka Tanzania, hivyo
kutoa fursa ya watangazaji wa China kujifunza lugha ya Kiswahili,” anasema Xie.
Xie anaongeza kuwa, China ni nchi inayoendelea kukua
hivyo watajitahidi kuwekeza nguvu zao katika kutangaza na kurusha matangazo kwa
lugha ya Kiswahili ili wananchi wa Afrika Mashariki waweze kujua mambo mengi ya
nchi hiyo.
Anasema, CR1 wamejipanga kuanzisha jarida la lugha ya
Kiswahili mbalo litakuwa likitoka kila baada ya miezi minne, hivyo ni fursa ya
ajira kwa waandishi wa lugha hiyo ya Kiswahili.
Xie anasema mbali ya jarida hilo kupatikana nchini China,
kwa Afrika litakuwa likipatikana nchini Rwanda, DR Congo, Kenya, Burundi na
Tanzania, nchi zinazozungumza zaidi Kiswahili.
“Jarida hilo ambalo litakuwa likisambazwa katika nchi
za Afrika Mashariki ambapo tumelenga kueleza habari mbalimbali zinazohusu
China pia litakuwa likitoka China ili kutoa elimu kuhusu bara la Afrika
ili Wachina wengi waweze kutambuana zaidi Afrika na Waafrika kwa ujumla,”
anasema Xie.
Mwandishi wa makala hii ambaye alikuwa kwenye
ziara hiyo aliweza kung’amua historia fupi ya Redio China iliyoanzishwa
kabla nchi hiyo haijapata uhuru kutoka kwa koloni lake Japan na hivi sasa
inatangaza kwa lugha tofauti zaidi ya 68 alisema Xie.
Xie anaongeza kwa kusema kwa mara ya kwanza walianza
kurusha matangazo yao mwaka 1949 kwa lugha ya Kijapani ambapo
taifa hilo lilikuwa halijapata uhuru wake kutoka kwa Mjapani.
Baada ya hapo, kituo hicho kiliendelea kupanuka na
kuanza kuongeza matangazo katika lugha mbalimbali duniani na
hadi ilipofika mwaka 1993, ndipo wakaanzisha Idhaa ya Lugha ya
Kiswahili.
Anasema, hivi sasa wamekuwa wakirusha matangazo mara
nne kwa siku ya lugha hiyo huku wakijiandaa na kurusha matangazo ya moja
kwa moja ya Kiswahili.
Aidha, Xie anafafanua kuwa moja ya matatizo ya lugha
ya Kiswahili, ni kasumba yake ya kuwa na maneno mengi yenye maana zaidi ya moja
tofauti na Kichina ambapo neno refu, huwa na maana moja na fupi.
Naye mtangazaji mkongwe wa Redio Tanzania hivi
sasa TBC Redio; mmoja wa watangazaji mahiri wa redio hiyo, Fadhili
Mpunji anasema vyanzo vya habari wanavyovitumia katika kupata habari, ni
Shirika la Habari la Xinhua.
“Hivi sasa redio yetu CRI, tunasikika katika matangazo
ya FM katika Radio 91 kote duniani. Hili ni jambo la kujivunia kwani
lugha ya Kiswahili inazidi kusikika katika nchi hizo duniani,” anasema Mpunji.
Mpunji anaongeza kuwa, nchini China hakuna chombo cha
habari kinachomilikiwa na mtu ama taasisi binafsi kama ilivyo kwa nchi nyingi za
Afrika (ikiwamo Tanzania), kila chombo cha habari kinamilikiwa na
serikali.
0 Comments