CHOKI NYAMWELA WATAMBULISHWA TWANGA PEPETA




Kutoka kushoto ni Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta  Luizer Mbutu akizungumza na wandishi wa habari hawapo pichani anayefuata mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini Ally Choki na Hassan Mussa 'Super Nyamwela ambao wametangazwa kujiunga na bendi ya Twanga wakiwa na Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka katika mkutano uliofanmyika kwenye hoteli ya Nemax Kinondoni Jijini Dar es Salaam leo.
 Luizer Mbutu akimtambulisha Super Nyamwela kuongeza nguvu katika safu ya wanennguaji wa bendi ya Twanga Pepeta.

Hapa ni baada ya  mkutano na waandishi wa habari kumalizika.


MWANAMUZIKI mkongwe nchini Ally Choki  mwenye majina mengi kama 'mzee wa Farasi', 'Mzee wa Kijiko' , 'Camarade' leo saa tano asubuhi ametangazwa kujiunga rasmi kujiunga na bendi ya Twanga Pepeta.

“Utambulisho huo ulifanyika chini ya Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta Luizer Mbutu  kwenye hoteli ya Nemax iliyopo Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Tumeamua kuiboresha bendi yetu mama Twanga Pepeta na huu ni uamuzi wangu binafsi sikushurutishwa na mtu yeyote ieleweke hivyo” alisema Choki.

Aidha akizungumzia kuhusu namna alivyojipanga upya katika bendi hiyo Choki alisema mashabiki wakae mkao wa kupata burudani ya aina yake na kisasa zaidi kwani amejipanga vilivyo kulikamata soko hasa akiwa na bendi ya Twanga Pepeta.

“Twanga  ni bendi yangu hakuna ubishi ni bendi ambayo nimeitumikia kwa miaka mingi sana hivyo kwa kuanzia nitatoka na kibao kitakachokwenda kwa jina la   ‘Kichwa Chini’ ambapo tutashirikiana na Luizer katika kuimba wimbo ambao unatoa somo kwa wanaume” alisema Choki .

Aliongeza kwa kusema kuwa pia tayari kuna nyimbo zingine mbili kali ambazo watazifyatua baadaye huku akiwataka mashabiki kuwa na subira.

Nyimbo hizo ambazo ziko jikoni ni pamoja na ‘Usiyaogope  Maisha’, ‘No Discuss’ alisema.

Akizungumzia juu ya ujio wake katika bendi hiyo alisema kwamba huo ni uamuzi wake binafsi wala hakuna shinikizo kutoka kwa mtu yeyote. 
“Unajua unaweza kuwa na kitu halafu ukashindwa kukimudu , hivyo hata wakati nilipokuwa nakaribia kwenda nchini Japan kwa mwaliko maalum wa kikazi niliwaambia wanamuziki wangu wa Extra Bongo kwamba nikirudi wajitayarishe nitatoa maamuzi magumu ya bendi lakini wakati nikiwa huko nikapata taarifa kwamba wameamua kila moja kutimka kwenda katika bendi ya Mwinjuma Muumini nawatakia kheri” alisema Choki.

Choki aliongeza kwa kusema kuwa  mkataba wake na bendi hiyo unamruhusu kufanya kazi nje ya bendi (Solo Artist) endapo mtu atamuhitaji akatoe burudani. 

“Mkataba wangu ndani ya bendi una maslahi mazuri na umekuwa wa kisasa zaidi hivyo hata kama kazi itatokea nje ya nchi ninabaraka zote za uongozi kufanya kazi za nje” alisema Choki.   

Akizungumzia kusambaratika kwa Extra Bongo alisema "Wanamuziki wa Extra Bongo walisambaa wenyewe na hii ilitokana wakati nasafiri nikaamua kuvifungia vyombo vyangu sababu hakukuwa na mtu ambaye niliyemuamini kumuachia mali yangu" alisema.

Aliongeza kwa kusema kwamba hatarajii kuasisi tena bendi kwa sababu hataki kuwa na ‘stress’kwa sababu kumiliki bendi ni pasua kichwa hivyo hataki kumfikiria mtu anataka kujifikiria yeye watoto wake na familia yake tu.

Mbali ya Choki pia mnenguaji Mussa Hassan ‘Super Nyamwela ’ na yeye amerudi katika bendi hiyo rasmi kama mnenguaji. 

Nyamwela alikuwa muasisi  na nyota wa  safu ya wanenguaji  bendi hiyo akiwa na waliokuwa wanenguaji nyota ambao wameshatangulia mbele ya haki  marehemu Halima White na Aisha Mbegu ‘Aisha Madinda’. 

Nyamwela alisema kwamba wao kama wasanii walitoka katika bendi hiyo na kwenda nje kutafuta maisha  hivyo masiha yakishindikana ni ruksa kwao kurudi nyumbani kama jinsi ilivyo sasa  wameamua kurudi nyumbani.

Kiongozi wa Twanga Pepeta Luizer alisema kwamba baada ya kupokea maombi kutoka kwa wapenzi wa bendi hiyo wameandaa onyesho maalum la kuwatambulisha litakalofanyika Aprili 18 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.  

Post a Comment

0 Comments