Na Mwandishi Wetu
KAMPENI maalumu za kupinga mauaji ya watu wenye u-albino nchini inayojulikana kama 'Imetosha' iliyoanzishwa na balozi wa kujitolea, Henry Mdimu, chini ya Imetosha Foundation zimezidi kushika asi baada ya makampuni ya IPTL na PAP kutoa shs milioni 10 kusaidia kampeni hizo.
Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa Makampuni ya IPTL na PAP, Bw. Joseph Makandege jana alimkabidhi balozi Mdimu mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 10 kama ishara ya kuunga mkono kampeni hizo za kutoa elimu kutokomeza imani potofu zilizojengeka kwa baadhi ya wanajamii juu ya watu wenye albino.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi Bw. Makandege alisema matukio ya mauaji au kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi yaani albino yamefika hatua ya kutisha nchini Tanzania, hususani katika kanda ya ziwa hivyo kuna kila sababu kila mmoja bila ubaguzi kushiriki kusaidia mapambano hayo.
Alisema ulemavu wa ngozi waliyonao watu wenye albino ni mapungufu ya kibaiolojia ambayo ni mapenzi ya Mungu hivyo imani potofu zinazoendelea hazina budi kupigwa vita kwa nguvu zote.
"...Kuna minongono mitaaani kwamba watu wanatenda matukio hayo wana imani potofu kwamba ukitumia kiungo cha mtu mwenye albinism, ndipo utafanikiwa. Kama kweli viungo vyao vingekuwa vinaleta utajiri, basi watu wenye albinism wangekuwa matajiri namba moja duniani," alisema Makandege akizungumza.
"...Sisi IPTL na PAP tumeguswa sana na jambo hili. Kwa wote wanaofanya matendo haya, mnapaswa kuwa na hofu ya Mungu mkijua kuwa siku ya kihama, kila mtu atajibu na kuhukumiwa kwa matendo yake. Tunakubaliana kabisa na wenzetu IMETOSHA Foundation kwamba, imefika wakati kila Mtanzania, na hata wageni waishio Tanzania, kusema IMETOSHA na kusimama kidete kuwalinda hawa ndugu zetu," alisisitiza kiongozi huyo wa IPTL.
Aidha kampuni za IPTL na PAP zimeyataka makampuni mengine nchini na watu binafsi kuungana kwa kuchangia harakati hizi za imetosha ili kusaidia kampeni ya imetosha kupita mikoa ya kanda ya ziwa kupaza sauti na kuielimisha jamii juu ya uwepo wa imani potofu zinazoendeleza mauaji ya watu wenye u-albino.
Kwa upande wake Balozi wa Imetosha, Mdimu aliishukuru kampuni za IPTL na PAP kwa moyo wauliouonesha wa kusaidia harakati hizo na kumtaka kila Mtanzania kwa nafasi yake kusaidia kupaza sauti kwamba imetosha mauaji na unyanyasaji wanaoupata watu wenye ualbino. Alisema mauaji haya yanamgusa kila Mtanzania na kuendelea kuichafua nchi yetu hivyo kumtaka kila mmoja kupaza sauti yake kupinga vitendo hivyo.
Machi 28, 2015 Imetosha Foundation inatarajia kufanya matembezi ya hisani kuchangisha fedha zaidi ili kusaidia kampeni za kukomesha mauaji ya watu wenye u-albino kabla ya kuanza rasmi safari za kuzunguka katika mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na wasanii waliojitolea kueneza elimu hiyo kwa jamii moja kwa moja.
0 Comments