BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde Ngoma ya Ukae'
inatarajia kuzindua albamu yake mpya ya 'Jinamizi la Talaka' mwishoni mwa
Oktoba baada ya kushindwa kufanya hivyo mwezi uliopita.
Baada ya uzinduzi huo bendi hiyo inatarajiwa kufanya ziara ya kimuziki
katika mikoa ya Morogoro na Dodoma kwa ajili ya kuzitambulisha nyimbo zao
mpya za albamu hiyo kwa mashabiki wa mikoa hiyo.
Msemaji Msaidizi wa Sikinde, Emmanuel Ndege alisema jana jijini Dar es
Salaam
kuwa baada ya kukwama
kufanya uzinduzi wao Agosti kama ilivyokuwa imetangazwa, Sikinde sasa
inatarajiwa kuzindua albamu yao mpya katika maadhimisho ya miaka 38 ya
kuanzishwa kwa bendi hiyo.
Ndege alisema kwa sasa wanaendelea kufanya mchakato wa wadhamini kabla ya
kutangaza rasmi tarehe ya jambo hilo, japo alisisitiza itakuwa mwishoni
mwa Oktoba.
"Uzinduzi wa albamu yetu mpya utafanyika Oktoba sambamba na maadhimisho
ya miaka 38 tangu kuanzishwa kwa Sikinde," alisema Ndege.
Pia aligusia juu ya ziara ya kimuziki wanaotarajia kuifanya wiki ijayo
katika mikoa ya Morogoro na Dodoma ili kutambulisha nyimbo zao mpya kwa
mashabiki wa bendi hiyo wa mikoa husika.
"Tupo katika maandalizi ya kwenda kuzitambulisha nyimbo za albamu yetu
mpya katika mikoa ya Dodoma na Morogoro, tukiwa huko pia tutakumbushia
nyimbo za zamani za bendi hiyo zilizoipa Ubingwa wa Muziki wa Dansi
Tanzania," alisema Ndege .
0 Comments