HAMZA KALALA AIBUKIA 'UTALII BAND'


MWANAMUZIKI mkongwe Hamza Kalala ametua rasmi katika bendi ya Utalii yenye maskani yake Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mmoja wa wakurugenzi wa bendi hiyo Injinia Augustino Kowelo alisema kuwa Kalala atakuwa  kiongozi  wa bendi hiyo ambayo tayari ina albamu moja.

Alisema lengo la kumchukua Kalala ni kuimarisha kundi lao kwa ajili kuutangaza utalii wa ndani kwa Watanzania hapa nchini.

Naye Kalala alisema kuwa ameamua kujiunga na kundi hilo baada ya kupiga kwa muda mrefu muziki wa kawaida.

Aliwataka wapenzi wa muziki kukaa mkao wa kula ili kupata vitu vikali kutoka katika kundi hilo lenye wasanii wote wa Tanzania ili kuutangaza vizuri utalii wa Tanzania.

Alisema kuwa tayari kundi hilo limetoa albamu ya kwanza inayojulikana kama Tembelea Hifadhi Zetu yenye nyimbo za Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ruaha na Manyara.
Wakati nyimbo zitakazokuwa katika albamu ijayo ni pamoja na Usichezee kazi chezea Mshahara, Ajali Mbaya na Mambo ya Town, ambazo ni moto wa kuotea mbali.

Mbali na Kalala wanamuziki wengine wa kundi hilo ni Omary Seseme (solo), Rashid Sumuni (solo),Duncan Ndumbalo (rhythm), Juma Zegezo (bass0, Stephen Muzenga (drums), Seleman Hamad (tumba), Moshi Hamisi (keyboard), James Mulamba, Melody Mbasha, Elibariki Kunukula (waimbaji).

Post a Comment

0 Comments