MISS KANDA MASHARIKI VIPAJI KUFANYIKA IDD PILI MAISHA PLUS KIBAHA

Baadhi ya washiriki wa shindano hilo wakiwa katika picha ya pamoja.

WAREMBO 14 wanaowania taji la Kanda ya Mashariki  ‘Redds Miss Eastern Zone 2014’  watashindania taji la vipaji ‘Talent Award’ lililopangwa kufanyika siku ya Idd Pili kwenye ukumbi wa Maisha Plus (Police Mess)  Kibaha, Mkoa wa Pwani. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam  jana, Mratibu wa mashindano hayo, Alex Nikitas alisema kuwa kutokana na mashindano hayo ya vipaji, kambi ya warembo iliyopangwa kuanza Julai 29 kwenye hotel ya Usambara Safari Lodge, sasa itaanza Julai 28 kwenye hotel ya Precision mkoani Pwani.

Nikitas alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekwisha kamilika na warembo hao mbali ya kushindana katika vipaji, pia watatoa msaada kwa kituo cha watoto yatima cha mkoa wa Pwani na baadaye kurejea mkoani Morogoro tayari kwa mashindano yaliyopangwa kufanyika  katika hoteli ya Nashera Hotel Agosti 8. 

Alisema kuwa mashindano hayo yatashirikisha jumla ya warembo 14 kutoka mikoa minne ambayo ni Pwani, Lindi, Mtwara na mwenyeji, Mkoa wa Morogoro chini ya udhamini wa Redds Original, Zanzi Cream Liquer, Pepsi, Usambara Safari Lodge, Kitwe General Traders, Starwing Lodge, Nashera Hotel, CXC Africa, Sykes Travel, Sasa Saloon, Grand Villa Hotel, Shabibby Line na Clouds FM. 

Nikitas anawataja warembo hao  kuwa ni  Lucy Julius Diu, Prisca Mengi, Tarchisia Noback Mtui na Angel Shio ambao wanatoka Morogoro. Warembo wengine ni Elizabeth Tarimo, Lilian Andrew na Leila Abdul Ally ambao wanatoka mkoa wa Lindi ambapo kutoka Mtwara ni Nidah Fred Katunzi, Lightness Mziray na Nelabo Emmanuel.

Pia warembo kutoka Pwani ni Khadija Ramadhan Sihaba, Irene Rajabu Soka, Mary Mpelo na Arafa Shaban. Nikitas alisema kuwa warembo hao watakuwa kambini kuanzia Julai 29 kwenye hotel ya Usambara Safari Lodge chini ya Miss Kanda ya mashariki mwaka jana, Diana Laizer.

Post a Comment

0 Comments