WanaCUF watakiwa kutovunjika moyo na matokeo ya uchaguzi mdogo jimbo la Kiembesamaki






Na Khamis Haji , OMKR

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho wasivunjike moyo na matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiembesamaki na badala yake waendelee na juhudi za kukiimarisha chama, ili kiweze kukamata dola katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
Akifungua mkutano wa viongozi wa matawi, majimbo na Wilaya kwa Wilaya za Wete na Micheweni uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Maalim Seif amesema kilichotangazwa Kiembesamaki si matakwa ya wananchi, kwa vile  kimsingi wananchi wa jimbo hilo walisusia uchaguzi huo.
Maalim Seif amesema idadi kubwa ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi huo si wakaazi wa eneo hilo, ambao walichukuliwa katika maeneo mbali mbali, baada ya kubainika wananchi wenyewe hawatashiriki kwa sababu hawakuridhishwa na maamuzi yaliyochukuliwa hadi kufanyika uchaguzi huo.
“Kama kuna wananchi wa Kiembesamaki waliokwenda kupiga kura basi hawazidi 1000, wengi walichukuliwa katika maeneo tafauti, kama vile Makunduchi, Mtende, Kitope na Bumbwini na wakapelekwa kupiga kura huku wakilindwa na vikosi vya Serikali”, alisema Maalim Seif.

Post a Comment

0 Comments