BALOZI IDDI AKABIDHI HATI ZA UMILIKI WA MASHAMBA YA KILIMO KWA WAKAZI WA KIJIJI CHA NGURUWENI

 Baadhi ya wananchi na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni wakiwa katika mkutano maalum  ulioitishwa  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kukabidhiwa hati za umiliki wa mashamba ya kilimo katika maeneo yao.

 Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Hati ya umiliki wa shamba Bibi Josephine Yohana kwenye hafla maalum ya kumaliza mgogoro wa mashamba katika kijiji hicho. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE

 Balozi Seif akimpatia Hati Bwana Mohd Ali Pili ya kumiliki eneo la kilimo katika Kijiji cha Nguruweni  ambako kuliibuka mgogoro uliosababishwa na kuinbgizwa watu wasiohusika na maeneo hayo kwa kilimo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
*****************************************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatahadharisha Wakulima wa Viijiji vya Ndunduke, Nguruweni na Dole  kuhakikisha kwamba maeneo ya kilimo waliyokabidhiwa na Serikali kwa shughuli za Kilimo wanayatumia  kama yalivyopangwa na kukubalika na pande hizo mbili.
Wakulima hao wakaonywa kuwa  ye yote atakaeamua maeneo hayo kuyakata viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuyauza kwa mtu mwengine aelewe kwamba Serikali italazimika kumnyang’anya mkulima huyo mara moja.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi hati  za umiliki wa mashamba ya kilimo kwa ajili ya wakulima 40 kati ya 181 wa Kijiji cha Nguruweni waliokuwa wakiilalamikia Serikali kwa kipindi kirefu kuidhinishiwa  mashamba wanayoyatumia ili kuendeleza shughuli zao za Kilimo.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya watu wenye tabia ya kuomba mashamba au eka kwa kisingizio cha kuendeleza kilimo lakini badala yake hujenga  tamaa inayowaelekeza kuanza kukata viwanja na kuuzia watu wengine.
“ Nataka nitahadharishe kabisa kwamba Mkulima ye yote atakayediriki kutumia fursa aliyopewa na Serikali ya kuendeleza kilimo kwenye shamba alilokabidhiwa na akaamua kufanya vyengine afahamu kwamba Serikali haitasita kunyang’anya shamba hilo mara moja “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwapongeza wakulima hao wa Nguruweni kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouchukuwa kwa kipindi kirefu kufuatia mgogoro wa maeneo waliyokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo baadhi yake kupewa watu wengine.
Balozi Seif alisema ustahamilivu huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuendeleza amani na utulivu kwenye Vijijini hivyo vya Nguruweni, Ndunduke pamoja  na Dole ambayo imeleta faraja kwa Serikali Kuu kwa vile haikuathiri shughuli za kila siku za kijamii.
Aliwakumbusha wakulima hao kwamba hivi sasa ni muda muwafaka wa kuendeleza shughuli zao za kilimo kwa vile wameshakuwa na uhalali wa kufanya hivyo katika maeneo waliyopewa na Serikali.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikisisitiza na kuhimiza kilimo kwa vile sekta hiyo bado inaendelea kuwa muhimili Mkuu wa uchumi wa Taifa hili.
“ Serikali imekuwa ikihimiza na kusisitiza umuhimu wa kilimo. Lakini Mkulima hawezi kuendeleza kilimo bila ya kuwa eneo la kilimo, sasa kwenu nyinyi hili suala  linaonekana kuondoka “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati Maalum aliyoiunda kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi kwa kushirikiana vyema na watendaji wa Wizara za Kilimo na Ardhi na kuutatua mgogoro huo wa muda mrefu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Ali Juma alisema Taasisi za Kilimo na Ardhi zililazimika kufanya uhakiki wa kina ili kuwatambua wakulima halali waliokuwa wakistahiki kupatiwa hati hizo.
Nd. Ali alisema uhakiki huo ulioshirikisha pia Masheha wa Vijiji vilivyohusika na mgogoro huo vya Nguruweni Ndunduke na Dole umeibua wakulima wapatao 181 ambapo  wakulima 40 kati ya hao wamethibitika kupatiwa hati hizo kwa awamu ya kwanza.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili alieleza kwamba kazi ya uhakiki sambamba na uchambuzi kwa wakulima wa Kijiji cha Dole imeshaanza rasmi na inatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.
Akitoa shukrani zake Mwenyekiti wa Kamati  Maalum iliyounda  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozib Seif kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ya vijiji vya Nguruweni, Ndunduke na Dole Mh. Abdulla Mwinyi  alisema Wakulima wa Vijiji hivyo  wanapaswa kupongezwa kwa umahiri wao wa ustahamilivu kufuatia mgogoro huo wa mashamba kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Mh. Abdulla Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi amewaomba wale wakulima ambao bado mgogoro wao haujapatiwa ufumbuzi waendelee kuwa na subra kwa vile Serikali kupitia Uongozi wa Kamati hiyo unajitahidi katika kukamilisha mchakato huo.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Wakulima hao Mmoja wa Wazee wa Vijiji hivyo Mzee Kitwana  Mustafa alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ujasiri na uungwana wake aliouchukuwa wa kutimiza ahadi aliyowapa  mwaka jana wa kumalizika kwa kadia hiyo.
Mzee Kitwana alisema wakulima wa Vijiji hivyo wamefarajika na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwatatulia kero lililokuwa likiwasumbua kwa miaka mingi iliyopita.
“ Ile furaha yetu tuliyonayo leo kama tumengeruhusiwa basi tunatamani tukubebe na matope yetu Mzee wetu kwa jinsi ulivyotujali na kututhamini  kwa katambua kwamba tulikuwa tukisumbuka kweli kweli “ Alionyesha furaha yake Mzee Kitwana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwahi kutoa  ahadi kwa wakulima hao wa Nguruweni, Ndunduke na Dole  kwamba Serikali  itayagawa maeneo  yote ambayo kamati aliyoiunda tarehe 14 Disemba Mwaka 2012 Chini ya Mwenyekiti wake Mh. Abdulla Mwinyi  kufanya uhakiki wa mashamba yote yaliyoleta mgogoro.
Wakulima hao waliwahi kutoa shutuma kali kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif dhidi ya watendaji na Maafisa  wanaosimamia Ardhi, Kilimo wakiwemo pia Viongozi wa ngazi ya kati wa Serikali kwa vitendo vyao vya kuingiza wakulima waliokuwa hawahusiki na mashamba hayo.
Watendaji hao walituhumiwa na wakulima hao kuvuruga  jukumu  walilopewa la kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya kwanza waliokubalika kupatiwa hati za umiliki huo chini ya aliyekuwa waziri Kiongozi wa mwisho wa SMZ  Mh. Shamsi Vuai Nahodha.
 Serikali ililazimika kuzuia utolewaji wa hati hizo kufuatia hitilafu zilizojichomoza za kupandikizwa baadhi ya watu wasiohusika jambo ambalo lilisababisha mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima hao na watendaji waliopewa jukumu la kusimamia suala hilo.

Post a Comment

0 Comments