Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akijadili na Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) Asteria Mlambo pamoja na watendaji
wengine umuhimu wa kufanyika mkutano wa pamoja ili kuweza kutatua
changamoto zinazojitokeza wakati ziara yake ya kukagua ujenzi wa
barabara ya magari yaendayo kwa kasi katika barabara ya Morogoro hadi
Sokoine.
Picha
juu na chini ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART)
Asteria Mlambo (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa Mstahiki Meya
wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo.
Muonekano
wa Barabara ya Morogoro ambayo bado inayoendelea kukarabatiwa kwa ajili
ya magari yaendayo kwa kasi ambayo imekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara
na pia sasa imegeuka kuwa njia maarufu ya Bodaboda zinazoendeshwa kwa
kasi na kuwa hatari kwa watembea kwa miguu ambao wamekuwa wakigongwa
katika barabara hiyo.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa akizungumzia changamoto
zinazojitokeza kufuatia ujenzi wa barabara ya Morogoro ambapo
limejitokeza suala la wafanyabiashara kuona kwamba itakapo kamilika
magari madogo yatakuwa hayapiti tena barabara hiyo hivyo hawajui hatma
ya biashara zao haswa kuanzia Bibi Titi hadi Sokoine na kusema iko haja
ya kukaa na wafanyabiashara hao kuwaeleza kuwa maendeleo hayakwepeki.
Akijibu
baadhi ya kero na maswali ya wakazi wa jiji kuhusu kucheleweshwa na
kuvurugwa kwa taratibu za barabara hiyo, Mstahiki meya amesema hiyo
inatokana na watu haswa wafanyabisha kujijengea miundo mbinu bila
kufuata taratibu za jiji, kitu ambacho kimesababisha mkandarasi
anapofanya kazi yake anakutana na mitaro, bomba za maji safi na taka,
mikongo ya mawasiliano ambazo haziko kwenye ramani na hapo lazima
awatafute wahusika nao wanataratibu zao hivyo kuwa kikwazo kwake
kukamilisha ujenzi huo.
Mmoja
wa wafanyabiashara wa eneo hilo Andrew John Shayo akielezea malalamiko
yao kuwa tangu ujenzi wa barabara hiyo uanze biashara hazifanyiki kwa
kuwa magari madogo hayapiti pia kumekuwa na tatizo la kupatikana kwa
maji kutokana na mkandarasi huyo kukatakata mabomba ya DAWASCO na kuwa
pindi mvua zinaponyesha maji yamekuwa hayaendi na kusababisha madimbwi
na kushauri ukarabati huo uharakishwe kwa kuwa wao ndio waathirika
wakubwa wa ujenzi huo.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) Asteria Mlambo akifafanua
kuwa mradi huo una mafungu saba ya utekelezaji na kati ya hayo fungu la
saba lilishakamilishwa ambalo ni uhamishaji wa nyaya za Umeme lakini
Kandarasi kuu tuliyonayo sasa hivi ambayo inawagusa watu wengi wa Dar es
Salaam ni ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, na kuwataka watu kuwa
wavumilivu kwa kuwa mkandarasi anashughulikia kwanza barabara kutoka
Kimara hadi Kivukoni.
Picha
Juu na chini ni Mstahiki Meya Jerry Silaa akiwa katika eneo lenye
dimbwi la maji ameshauri Ili kupunguza msongamano tunafanya utaratibu
angalao sasa tufungue barabara za India, jamhuri, Libya ili angalao
kupunguza msongamano wa upande mmoja wa mji lakini baadae itabidi
kujadiliana ili ujenzi huu ukikamilika mwezi Juni kutakuwa na changamoto
za aina gani kwa pamoja na viongozi wa mitaa, wafanya biashara, wenzetu
wa DART ili tuone biashara za watu zitaendelea kwa staili ya aina gani.
Amesema
hatuwezi kubaki na jiji lilelile la zamani lazima tubadilike, kwa mradi
wa kisasa kama huu Tanzania kwa maana ya jiji la Dar es Salaam ndio
litakuwa la pili barani Afrika, mradi kama huu mpaka sasa uko Afrika
Kusini peke. Na hizi barabara zinajengwa kwa kiwango cha zege hivyo
zinadumu kwa miaka mingi.
Na.Mwandishi wetu
Mstahiki
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jerry Silaa ameitisha mkutano
wa pamoja na wafanyabiasha, wadau na watendaji wa idara mbalimbali za
serikali ili kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (DART).
Mstahiki
Silaa amefikia uamuzi huo baada ya kujionea changamoto mbalimbali
zinazojitokeza wakati wa mradi huo katika makutano ya barabara za Bibi
Titi na Morogoro hadi barabara ya Sokoine ambazo zimekuwa kero kubwa kwa
wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.
Akizungumza
baada ya kufanya ziara ya mradi huo katika barabara hizo, Silaa amesema
kuna haja ya kuwepo kwa mkutano wa wadau mbalimbali kutoka Shirika la
Nyumba (NHC), Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO), Mamlaka ya Mapato
Nchini (TRA) na wafanyabiashara katika maeneo ya mradi huo ili kujadili
na kufikia muafaka wa pamoja wa kutatua changamoto hizo.
Meya
huyo amesema changamoto ni nyingi lakini zinaweza kutatuliwa ikiwa
wadau wote wanaohusika katika mradi huu watakutana na kujadili kwa kina
njia na hatua stahiki za kukabiliana na changamoto hizo.
Amezitaja
changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa mradi huo kuwa ni pamoja na
kuongezeka kwa foleni baada ya njia nyingi kufungwa, kukosekana mahala
pa kuegesha magari, kutokuwepo na njia za kupitisha magari ya zima moto
na uharibifu wa miundombinu ya maji wakati wa ujenzi wa barabara.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART),
Asteria Mlambo amesema kuwa pamoja na changamoto hizo zinazojitokeza
wakati wa utekelezaji wa mradi lakini jitihada za makusudi zinafanyika
kuzitatua hasa zile zilizo ndani ya uwezo wetu.
Amesema
mwenendo wa mradi huo unakwenda katika malengo yaliyopangwa kulingana
na makubaliano ya mkandarasi wa mradi huo Strabag ili kutekeleza ahadi
yake kwa Serikali ya kukamilisha mradi huo hadi ifikapo mwaka 2015.
Ameongeza
kuwa utekelezaji wa mradi huu unaendelea vizuri pamoja na changamoto za
hapa na pale, tunaomba ushirikiano wa wananchi na watumiaji wa barabara
kwa ujumla kuheshimu na kufuata maelekezo ya barabarani yanayowakataza
kutumia barabara zilizo kwenye matengenezo.
0 Comments