TAMASHA LA PASAKA LAPATA KIBALI

ALEX MSAMA PICHANI.
Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Pasaka la mwaka huu 2012 linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions, limepata kibali kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu wa tamasha hilo, Alex Msama alisema kibali kilitolewa juzi kwa ajili ya tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Aprili 8 mwaka huu, Dar es Salaam.

Msama alisema taratibu za maandalizi ya tamasha hilo zinaendelea ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na baadhi ya waimbaji wa nyimbo za Injili watakaotumbuiza, na pia kupata mahali ambayo litafanyika.

"Pia tunaendelea na taratibu za kumpata mgeni rasmi na uwanja utakaotumika kwa tamasha hilo kwani mwaka jana tulibaini ukumbi wa Diamond Jubilee ulikuwa mdogo na watu wengi waliofika walikosa nafasi ya kushuhudia," alisema Msama.

Mwaka jana mashabiki walikuwa mara tatu zaidi ya ilivyotarajiwa huku nusu ya watu waliofika kushuhudia tamasha hilo wakikosa nafasi ya kuingia ndani na kubaki kushuhudia kupitia milango ya ukumbi huo.

Kutokana na hali hiyo, Msama alisema tamasha hilo lilikuwa la mwisho kufanyika kwenye ukumbi huo na mwaka huu atafanya ama kwenye Uwanja wa Taifa au Mnazi Mmoja.

Mgeni rasmi katika tamasha hilo mwaka jana alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, na lengo lilikuwa ni kusaidia watu wasiojiweza, wajane na walemavu, azma ambayo ilitimizwa.

Msama alisema tamasha hilo si la kibiashara, akaomba Basata kupunguza gharama ili liwe na waimbaji wengi kutoka nje ya nchi ikiwa ni moja ya njia ya kudumisha umoja baina ya Tanzania na nchi jirani.

Rais Kikwete aliwaeleza Basata kutekeleza ombi hilo kwani kazi inayofanywa na Kampuni ya Msama Ptomotions ya kusaidia makundi ya watu wasiojiweza ni kubwa na linapojitokeza tatizo la kuhitaji msaada wa kulifanikisha, Serikali inatakiwa kuonesha msaada wake.

Rais Kikwete alisema nyimbo ni silaha nzuri ya kutumika katika jamii ambayo hata kwenye nyanja ya siasa hutumika kuwakutanisha wananchi na sanaa ya muziki ina kazi ya ziada ya kusoma maisha ya kawaida ya jamii kwani huelezea historia ya maisha yao.

Post a Comment

0 Comments