BASATA YATAKA WASANII KUJIKITA KWENYE SANAA ZA ASILI

 Akina mama wapiga ngoma kwenye Kundi la Chabwede wakiwajibika vilivyo wakati wakitoa burudani kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA wiki hii. 
  Wacheza ngoma wa Kundi la Chabwede wakionesha vitu vyao kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu makao makuu ya BASATA, Ilala Sharif Shamba.
 Sehemu ya wadau waliohudhuria Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifurahia burudani iliyokuwa ikiporomoshwa na Kundi la Ngoma za Asili la Chabwede.

Na Mwandishi Wetu.
BARAZA  la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujikita kwenye ngoma za asili huku likitoa wito kwa wasanii wakongwe katika fani hiyo kuirithisha kwa watoto.

Wito huo umetolewa wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Ghonche Materego mara baada ya kushuhudia burudani ya kuvutia iliyoporomoshwa na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Chabwede kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA.

Alisema kuwa, kwa sasa ngoma nyingi za asili zinateteleka kutokana na wasanii kujikita kwenye fani nyingine au kujiingiza kwenye sanaa za kisasa hivyo kuhitajika juhudi za makusudi katika kurithisha sanaa hii kwa watoto lakini pia wasanii kutumia vionjo vya asili katika kazi zao.

“Hapa tumeambiwa ngoma kama za Segere na Mdundiko zinaanza kupotea, ni lazima vikundi vya ngoma vihusishe watoto ili waweze kurithi” alisema Materego.

Aliongeza kuwa, kuna haja ya wasanii kuanza kujiuliza na kuzijaribu ngoma za asili kwenye kazi zao, ili kuona ni kwa kiwango gani zinatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine lakini pia kuleta vionjo tofauti katika kazi zao.Katika kuunga mkono harakati za Kundi la Chabwede katika kukuza fani ya ngoma za asili, BASATA ilitoa ngoma tatu za kisasa.

“BASATA tunatambua juhudi za kundi hili, katika kuliunga mkono zaidi na kuungana nalo katika kazi zao, tunalipatia ngoma tatu za kisasa” aliongeza Materego.

Awali akizungumza na Wadau wa Jukwaa la Sanaa baada ya kutoa burudani, Katibu wa Kundi hilo linalofanya kazi zake eneo la Kijiji cha Makumbusho Anna Said Tindima alisema kuwa, kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakidharau ngoma za asili hali inayodidimiza fani hiyo.

Aliongeza kuwa, kuna kila sababu ya vijana kurudi kwenye asili zao na kujihusisha kikamilifu na sanaa zinazopatikana maeneo yao ili kuhakikisha hazipotei.

Post a Comment

0 Comments