MAANDALIZI YA SHEAR CHARITY BALL 2011 YAANZA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
Tafrija ya hisani ya Shear kuchangisha Tsh. Milioni 50 kusaidia wanawake walioathirika na fistula na kwa ajili ya kukarabati na kuimarisha mfumo wa maji safi na majitaka katika hospitali ya Amana.
Dar es Salaam, Tanzania - Septemba 7, 2011JARIDA la urembo na mitindo ya nywele la Shear (Shear Hair & Beauty Magazine) linaadhimisha miaka miwili ya kuwapo katika biashara kwa kuandaa tafrija ya hisani yenye lengo la kuchangisha fedha zitakazowezesha kufanyika kwa upasuaji wa bure kwa wanawake wanaosumbuliwa na maradhi ya fistula katika hospitali ya CCBRT sambamba na kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika hospitali ya Amana.Tafrija hii ya hisani itafanyika Oktoba 1, 2011 kuanzia saa 1:00 usiku katika ukumbi wa Kivukoni uliopo kwenye hoteli ya Movenpick Royal Palm.Katika tafrija ya kwanza iliyofanyika mwaka jana katika hoteli ya Double Tree by Hilton, kiasi cha shilingi milioni 15 kilichangwa na nusu ya fedha hizo zikapelekwa CCBRT kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa fistula kwa wanawake waliokuwa na uhitaji wa tiba hiyo na kiasi kingine kikapelekwa katika Kijiji cha kulelea watoto cha SOS kilichopo Dar es Salaam ambako fedha hizo zilitumika kuchangia ada kwa watoto waliokuwa wakipata elimu katika kijiji hicho. Kupitia tukio hili, tumeamua kutoa elimu kwa umma kuhusu maradhi haya yanayotibika ya fistula ambayo kwa karne nyingine yamekuwa na athari mbaya katika utu wa mwanamke. Ni jambo la kheri kwamba, hospitali ya CCBRT imekuwa ikitoa tiba ya bure kwa wanawake na hivyo kuwarejeshea utu ambao umekuwa ukitishiwa na maradhi haya. Hospitali ya Amana kwa upande wake inakabiliwa na tatizo la maji inayosababishwa na uchakavu wa mabomba ya maji safi na maji taka, wenye uwezo mdogo wa kusafirisha majitaka hali inayoathiri ufanisi katika shughuli za usafi kwenye maeneo ya karibu na hospitali hiyo. Iwapo mfumo huo utaimarishwa, hospitali itaimarisha uwezo wake wa kutoa huduma bora na salama kwa wagonjwa na wafanyakazi na hivyo kudhibiti maambukizi kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.Hospitali ya Amana inahudumia wastani wa wagonjwa 1,500 kwa siku na watoto wapatao 100 wanazaliwa hapo kila siku. Hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la kukosekana kwa vyanzo salama vya maji na mfumo duni wa majitaka, hali ambayo ni ya hatari kwa utendaji kazi wake. Hospitali inahitaji kisima kimoja cha maji kitakachojengewa pampu ya kusukuma maji na kuboreshwa kwa mfumo wake wa majitaka ili kuimarisha hali hii mbaya iliyopo sasa. Tafrija hii ya hisani ya mwaka jana lilikuwa ni yenye mafanikio ya kutia moyo. Tunaamini jamii inaiunga mkono dhamira yetu hiyo njema na kuungana nasi tena katika tukio la Oktoba Mosi ili kusaidia kufikia malengo tuliyojiwekea.Tunapenda kuzishukuru taasisi zifuatazo ambazo tayari zimeonyesha dhamira ya kweli ya kusaidia malengo haya muhimu; Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirikia la Nyumba la Taifa (NHC), Billicanas Group, Fly540, MaxCom, Precision Air, DeskTop Production (DTP), Hoteli ya Peacock, Clouds Radio na Clouds TV, Kampuni ya vifaa vya ujenzi SS Concrete, Benki ya Azania, BenchMark Production, Advertising Dar, Pepsi, Tanzania House of Talent (THT), I-View Media, mafuta ya kulainisha ngozi CocoTan, duka la nguo la Tina Maria, Kampuni ya kupamba masherehe ya Hugo Domingo, Imaging Smart na taasisi nyingi nyingine za Dar es Salaaam. Tunapenda kuzitia moyo taasisi na watu wengine binafsi kujitokeza na kuchangia katika tafrija yetu hii ya hisani kwa kufika au kwa kuchangia ili kuifanya dunia iendelee kuwa sehemu nzuri na bora zaidi ya kuishi kwa wanawake wenye fistula ambao wanahitaji tiba na uangalizi wa CCBRT na wagonjwa kwa mamia wanaopata huduma katika hospitali ya Amana kila siku.Kuhusu Jarida la Urembo na Mitindo ya Nywele la Shear (Shear Hair & Beauty Magazine)
Jarida la Urembo na Mitindo ya Nywele la Shear (Shear Hair & Beauty Magazine) ndilo jarida kubwa na la kipekee linalohusu masuala ya urembo na mitindo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati. Jarida hili linalotoka mara moja katika kipindi cha kila miezi miwili, limejielekeza katika kupasha habari, kuelimisha na kuburudisha huku likichagiza kupitia machapisho yake ya msimu masuala muhimu yanayohusu jamii, afya ya wanawake, nywele, urembo na mitindo ya hapa Tanzania na kwingineko duniani. Jarida hili huja na dondoo za mitindo ya kisasa ya nywele za wanawake wa rika tofauti, kuanzia mabinti hadi wanawake watu wazima. Kila toleo lina ushauri wa kitaalam, mitindo ya ubunifu wa nywele, dondoo za urembo, huku likitoa mbinu za mahitaji ya wanawake katika kuboresha nywele, ngozi na afya ya mwili kwa ujumla. Jarida linakuwa pia na makala zinazohusu masuala yanayohusu wanamitindo wa hapa nyumbani, wabunifu wa mitindo huku likiwazungumzia watu maarufu wakiwamo wanamuziki na waigizaji wa filamu. Wanawake hawa maarufu wanaungana na wenzao wengine duniani wenye mitazamo na wanaohusudu mitindo inayofanana. Jarida hili ni kioo kwa wanawake wa mijini wanaopenda kujifunza kwa wepesi urembo unaofaa maofisini, na ule wa katika hafla mbalimbali kama za kijamii au harusi.Jarida hili la urembo na mitindo ya nywele linasambazwa katika miji yote mikubwa hapa nchini kwa malengo ya kuwasaidia wasomaji wake waweze kudurusu na kurejea masuala mbalimbali ya urembo na mitindo yampasayo mwanamke wa Kiafrika.Taarifa zaidi kuhusu tafrija hii unaweza kuzipata katika mtandao wa intaneti kupitia tovuti ya www.shearillusionstz.com au katika kurasa za matukio na katika facebook pia.
Unaweza ukapata tiketi na maelekezo mengine kwa kuwasiliana nasi kwa njia ya email yetu ya info@shearillusionstz.com/shearcharityball.html au kwa simu ya Dora +255 787 765533.
Tunatanguliza shukrani.
Shekha Nasser,
Mwenyekiti Kamati ya Maandalizi Shear Charity Ball Email: shekhanasser@shearillusionstz.com
Simu: +255 686 997 888




Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya  CCBRT Haika Mawalla kushoto,katikati ni Mwenyekiti wa Shear Charity Ball Shear Ball Shekha Nasser na  Mhanga Mkuu wa Hospitali ya Amana Dk.Shimwela.

Post a Comment

0 Comments