Na Dina Ismail.
Timu ya soka ya Yanga jana ilijiweka katika mazingira mazuri ya kuwapiku mabingwa watetezi Simba baada ya kuilaza Azam FC kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Uhuru ‘Shamba la Bibi’ jana jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na upinzani wa hali ya juu, iliwachukua wauza koni ‘Lambalamba’ Azam FC dakika mbili tu kucheka na nyavu za Yanga, baada ya John Boko ‘Adebayor’ kutupia nyavuni kwa shuti kali, baada ya kutumia vema makosa ya Nadir Haroub kuokoa mpira kwa papara na kumgonga mchezaji mmoja kabla ya mfungaji kuunasa na kufanya kweli.
Dakika ya 9, Mrisho Ngassa alipiga shuti kali lakini likadakwa na kipa Ivan Knezevic, kabla ya Yanga kujibu kwa shuti kali la Davis Mwape lililogonga mwamba dakika ya 12, huku Jerry Tegete naye akikosa mabao ya wazi matatu kutokana na kupiga mpira fyongo.
Yanga waliendelea kusaka bao la kusawazisha, ambako dakika ya 32 Kigi Makasi alipiga shuti kali lakini likatoka juu ya mwamba, kabla ya dakika ya 41 Tegete kurekebisha makosa na kupachika bao la kusawazisha baada ya kumpiga chenga kipa wa Azam.
Baada ya bao hilo, mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam alimzawadia Tegete kadi ya njano kutokana na utovu wa nidhamu.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa zimetoshana nguvu ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, ambako Ngassa alijikuta akilimwa kadi ya njano kutokana na kuzozana na mwamuzi Ndege.
Dakika ya 56, Tegete alikosa bao baada ya kupokea mpira wa krosi na kupiga shuti lililotoka nje. Wachezaji wa Azam FC, Redondo na Boko nao walizawadiwa kadi ya njano kutokana na mchezo mbaya.
Alikuwa Tegete tena ambaye alipokea mpira wa kurushwa na Mbuna na kupiga kichwa lakini kikapaa juu ya goli, kabla ya kusawazisha makosa na kupachika bao la pili kwa kuchwa akitumia vema pasi ya ya Mwape na kumtoka kipa Nyonzikuru.
Dakika ya 80 daktari wa Yanga alitolewa kwenye benchi kutokana na utovu wa nidhamu, huku Nurdin Bakari naye akizawadiwa kadi ya njano. Hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Ndege, Yanga ilitoka kifua mbele kwa mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 43 na kuzidi kuwapumulia watani zao Simba walioko kileleni kwa pointi zao 45 huku kila timu ikibakisha michezo miwili, hivyo kufanya ubingwa kubaki kuwa kitendawili. Azam FC imebaki na pointi zake 37.
Yanga: Ivan Knezevic, Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’, Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Chacha Marwa, Juma Seif/ Omega Seme, Fred Mbuna, Nurdin Bakari, Davis Mwape, Jerry Tegete, Kigi Makassy.
Azam: Vladimir Nyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/ Himid Mao, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Patrick Mafisango, Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, John Boko, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Suleiman Kassim/ Kally Ongala.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Mwandishi Wetu Ramadhani Siwayombe anaripoti kuwa, wenyeji AFC Arusha ambao tayari wamechungulia Ligi Daraja la Kwanza, walitoshana nguvu na Wakata Miwa wa Mtibwa Sugar kwa sare ya 1-1.
Mtibwa Sugar ilipata bao lao dakika ya 20 kwa njia ya penalti mfungaji akiwa mkongwe Monja Liseki, baada ya mchezaji mmoja wa Mtibwa kufanyiwa madhambi, kabla ya Dakika ya 24 na Abdallah Juma wa AFC kuisawazishia timu yake kwa shuti la karibu.
0 Comments