VITA YA ALLY CHOKI , ASHA BARAKA ITAUFIKISHA WAPI MUZIKI WA DANSI TZ?

MWISHONI wa wiki iliyopita Februari 5, 2011 vyombo vingi vya habari vilipambwa na taarifa kuhusu bendi ya Extra Bongo kuchukua wanamuziki sita kutoka bendi kongwe nchini ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ huku ikijitapa kwamba lazima itaendelea kuibomoa hadi waitoe roho bendi hiyo.
Kila mmoja nafikiri aliipokea taarifa hii kwa namna yake, kwa mtazamo wangu mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki, amefanya uonevu ingawa yeye hapendi kuonewa.
Namuona Choki kuwa ni mbinafsi, anayejijali binafsi na kujiona ndiye anayestahili kumiliki kitu chochote kizuri, huku akipenda kuona mabaya yakiwafika majirani zake wakiwemo wale wanaomzunguka.
Nikiri kuwa kitendo cha wanamuziki kutoka kwenye kundi hili kuhamia kwingine ni cha kawaida kabisa katika sanaa, hakikuanza leo, jana wala juzi.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwishoni mwa miaka ya 1970, kundi la wanamuziki kadhaa waliipa kisogo bendi ya Dar International iliyokuwa ikitikisa kwa wakati huo na kuingia DDC Mlimani Park; bendi inayopiga muziki wa dansi kama apigao Choki.
Mchezo huu wa kuchukuliana wanamuziki, hata hivyo, haukuanzia kwa Mlimani Park na Dar International wala kuishia hapo, uliendelea pia ndani ya Mlimani Park yenyewe, Msondo, OSS, Marquis Du Zaire na Orchestre Bima Lee.
Lakini nafikiri Choki haijui ‘Fair Play’ hii kwa sababu, miaka takriban sita nyuma alipoianzisha rasmi kwa mara ya kwanza bendi ya Extra Bongo na kufa baada ya miaka miwili alilalamika sana akidai amefanyiwa hujuma.
Lawama nyingi alizielekeza kwa uongozi wa kampuni ya The African Stars Entertainment ASET, hususan mkurugenzi wa Twanga Pepeta inayomilikiwa na kampuni hiyo, Asha Baraka - Iron Lady.
Hata alipoifufua upya Extra Bongo mwishoni mwa mwaka juzi, alitia msisitizo kuwa sasa yuko ngangari kinoma na fitna zozote zinazoweza kujitokeza dhidi yake hata zikiwa ni zaidi ya zile ‘zilizomuua’ wakati ule hazimtishi.
Mwaka mmoja baadaye akiwa kaachia albamu yake iliyotamba kwa jina la ‘Mjini Mipango’ mkung’utaji wake mahiri wa gitaa la Solo, Adam Hassan ‘Mkono wa Biashara’, akaipa kisogo bendi hiyo na kuhamia katika bendi ya Manchester Musica.
Tukasikia tena Choki akikasirika na kuja juu kama mbogo huku akitangaza vita kwa baadhi ya waandishi wa habari, akiwamo mwanasafu wa jarida hili la Wikiendi ambaye mimi nimembatiza jina la kumwita ‘Jembe Langu’ naye si mwingine bali ni Abdallah Menssah akidai anahusika na uondokaji wa mwanamuziki huyo.
Ni dhahiri kuwa hili la kuondoka kwa Adam Hassan lilimgusa na kumchoma vilivyo, lakini hatujakaa sawa naye akaona atulize jazba zake kwa kuwachukua waimbaji wa Twanga: Kalala Junior na Khalid Chokoraa ambao alipiga nao kazi katika mkesha wa kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha 2011 pale Vatican City Sinza.
Kwa kweli acha nisiwe mchoyo, vijana walipiga kazi. niliukaribisha mwaka katika ukumbi wa Makumbusho katika onyesho la bendi ya FM Academia na baadaye nikajitoma kwenye ukumbi wa Salender Bridge ambako bendi ya The Kilimanjaro ilikuwa ikipiga.
Niliyajua hayo kwa kupitia wadau na wanahabari wenzangu ambao walikwenda kumpa sapoti Choki siku hiyo.
Lakini licha ya kutowachukua kabisa vijana hao ambao kwa sasa wanapiga mzigo kwenye bendi yao ya Mapacha Watatu, kimya na utulivu wa kambi ya Twanga Pepeta kilimpa nguvu na kiu zaidi ya kutazama wengine ndani ya bendi hiyo inayotamba hivi sasa hapa nchini, ambayo makao yake makuu yako Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kama Waswahili wasemavyo mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe hivyo ndivyo Choki alipopiga fataki lake wiki moja iliyopita baada ya kuwanyakua tena wanamuziki sita wa Twanga kwa mpigo.
Na baada ya siku tano wapya hao kutua Extra Bongo aliyekuwa kiongozi katika bendi yake, Khadija Mnoga ‘Kimobitel’, pamoja na Grayson Semsekwa, wamebwaga manyanga na kurejea nyumbani ASET ambako wametambulishwa katika onyesho la Usiku wa Mwafrika unaolindima kila siku ya Jumatano kwenye ukumbi wa Kimataifa Club Builicanas jijini Dar es Salaam.
Wakati uongozi wa Twanga ukiwatambulisha kwa waandishi wa habari, Kimobitel aliweka wazi kuwa ameondoka Extra Bongo kutokana na kunyanyaswa na kutakiwa kutoa maamuzi mabaya huku yale mazuri yakifanywa na wenye bendi jambo ambalo alidai kwamba lilimuuma sana hasa pale alipotakiwa kuwafukuza kazi wanamuziki sita katika bendi ambao alidai ndio waliokuwa wastahmilivu katika Extra Bongo.
Kama muziki tukiulinganisha na maisha ya nyumbani, basi kwa hili la kumtaka Mnoga apunguze wanamuziki wa zamani, Choki angeweza kuamrisha familia kutupa vyungu vya zamani baada ya kupata vipya.
Lakini umefika wakati sasa kwake kutambua kuwa muziki ndivyo ulivyo hivyo na huu mtindo aliouanzisha siyo mzuri na haupendezi katika jamii kwani unaleta chuki.
Ukweli ni kwamba Twanga nao wakiamua kutafuta wafadhili na kuchukua wanamuziki wake hawatashindwa na hilo litamuuma.
Kama lengo lilikuwa ni kuboresha ngome ya Extra Bongo angefanya mseto kwani angeweza kuchukua wanamuziki katika bendi za FM Academia, Akudo, Stoni Mayasica na Diamond Sound.
Lakini kwa kubeba wanamuziki wa Twanga na kudai kuwa lazima atoe roho ya bendi hiyo, sidhani kama ni sahihi kwani hata muziki wenyewe utakuwa na ladha na vionjo feki vya Twanga wakati mashabiki watakwenda kupata kitu Original kwa Twanga wenyewe.
Hebu tuwatupie macho FM Academia wana muziki wao na ladha yao, ukienda katika bendi ya The Kilimanjaro nako ndiyo poteza mbaya utapata kitu kingine, nenda Jahazi utaridhika na kama haitoshi ukiingia Twanga utakuta nao wanavionjo vyao.
Kama haitoshi nenda La Prima kwa bendi ya Le Capital, Kalunde utapata kitu tofauti huo ndiyo ushindani wanaoutaka mashabiki lakini chuki na uhasama katika muziki havipendezi hata sisi wanahabari mnatukera na kutuyumbisha.
Katika kipindi cha mwaka jana bendi zote zilitulia sasa mnataka kutugawa wenyewe tena kwa makusudi kwa kuchukuliana wasanii.
Nachukua fursa hii kuwaeleza wanamuziki na wakurugenzi wa bendi zote wawe na mipaka katika kutafuta wasanii au wanamuziki wapya ili waepuke kujenga chuki na kuziathiri bendi nyingine.
Vinginevyo, nashauri kuanzishwe sheria mpya ambayo itazilazimisha bendi zinazochukua wanamuziki kutoka bendi nyingine kulipia ada ya uhamisho ili ifidie bendi iliyochukuliwa wanamuziki au wasanii wake. Huu ni utaratibu mzuri kama unavyotumika katika soka ambako kuna mawakala wanaouza na kununua wachezaji huku wakilipia ada ya uhamisho.

Post a Comment

2 Comments

Anonymous said…
Mimi sioni ajabu kwa wanamuziki kutoka bendi moja hadi nyingine,ni hali ya kutafuta maisha,jambo hili la wanamuziki kutoka Twanga kwenda Extra bongo imekuwa kama vile kitendo cha kinyama au cha uuaji !!!mbona Twanga huchukua wanamuziki ktk bendi nyinginezo na watu hawasemi??tena blog hii nimeifuatuilia kwa makini na kugundua kuwa inajipendekeza sana kwa Twanga,nadhani huwa inapata fungu fulani,na hii ni hali inayoshiria kuwa hakuna u profession unaoonyeshwa katika uandishi wa habari wa blog hii,muhariri jitahidi kuwa neutral katika habari zako bila kupendelea upande wowote,msidhani sisi wasomaji wa hizi blogs ni wajinga tunaangalia karibu stories zote mnazoandika huko bongo.Hakuna haja ya kumsakama Ally Choki,muziki ni ajira kama ajira nyingine,hii na sawa na fani yoyote ya sanaa au michezo watu wako free kujiunga na bendi au kikundi chochote na siyo kusakamwa sababu wametoka Twanga.Umetoa mfano wa Dar Int.,Sikinde,Safari sound nk.sasa ni lipi la ajabu waaaanamuziki kutoka Twanga ???acha kujipendekeza ktk upande mmoja,onyesha uhariri uliokomaa.Kama utaibania hii article yangu ni sawa tu.
mwanamuziki mkongwe Bahrain
Anonymous said…
Hadija Khalili kuwa muangalifu na upendeleo wako unaoonekena wazi unajipendekeza sana kwa African Stars,kuhama kwa wanamuziki ni jambo la kawaida,hii yote ni kutafuta maisha,hakuna mwanamuziki anayelazimishwa kukaa bendi moja milele,hakuna haja kabisa ya kuwalaumu wanamuziki waliotoka A.Stars wala kumlaumu kiongozi wa Extra bongo.PIa inabidi uonyeshe jamii jinsi ulivyo makini katika fani hii ya uandishi na siyo kupendelea upande mmoja kila mara.Hii siyo mara ya kwanza kuona wewe ukilalia sana upande wa Twanga,jaribu sana kureekebisha tabia hii au la tutaacha kabisa kusoma blog yako,kuwa fair na habari zote utoazo na siyo kila wakati kupendelea upande mmoja,
mdau Kariokoo,Dar