NCCR MAGEUZI YAWASHIKA PABAYA TAMWA & CHADEMA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama Cha NCCRR-Mageuzi,Bw. James Mbatia, ametoa siku saba kwa Chama Cha Wanahabari Wanawake (TAMWA)kumlipa fidia ya sh. Bilioni 1 kwa kumdhalilishwa.

Wakati huohuo, Bw. Mbatia ametoa siku tatu kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kumlipa sh. Bilioni 1 na kukilipa Chama Cha NCCR shilingi bilioni 3 kama fidia ya kudhalilishwa.

Mbatia alibainisha hayo jijini leo alipozungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya kisiasa katika wiki ya mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Aidha Mbatia alisema, TAMWA kupitia Mkurugenzi wake Bi. Annanilea Nkya imekuwa ikitoa taarifa za uzushi na uongo juu yake pia ikimtuhumu kumyanyasa mpinzani wake jimbo la Kawe Bi. Halima Mdee.

Alisema Taasisi hiyo inamtuhumu kutokuwa na hoja wala sera,kutumia lugha za matusi, kutumia mbinu chafu na kejeli,kuwa na mtazamo potofu juu ya mpinzani wake jimbo la Kawe, jambo ambalo ni uzushi.

"Nilikuwa naiheshimu sana TAMWA lakini kwa kunizushia kwamba nanyanyasa wanawake imeniuma sana... chama chetu kinatoa fursa sawa kwa wanaume na wanawake kama nembo ya chama chetu inavyoashiria, hata Makamu Mwenyekiti wangu ni mwanamke" alisema.

Aliituhumu TAMWA kuwa wakala wa CHADEMA hivyo kusambaza maneno ya uongo kwa vyombo vya habari, ambapo ametoa siku saba kwa chama hicho kumlipa fidia hiyo.

Katika hatua nyingine,Bw. Mbatia amekishukia chama cha CHADEMA,kwa kumdhalilisha kupitia mikutano ya kampeni inayofanywa na mgombea ubunge wa chama hicho jimbo la Kawe.

Bw.Mbatia alisema, Bi. Mdee amekuwa akimtuhumu kuwa kibaraka wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) na kupokea kiasi cha sh. milioni 80 kwa wiki kutoka chama hicho.

Alisema licha ya kufikisha malalamiko hayo katika Tume ya Maadili, tume hiyo haijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo.

Alisema, amefikia hatua hiyo baada ya mgombea Urais wa CHADEMA,Dkt. Wilibroad Slaa kuonesha kuunga mkono tuhuma zinazotolewa na Mdee wakati akihutubia katika Viwanja vya Tanganyika Peckers juzi.

Alisema kupitia mkutanao wa Dkt. Slaa chama chake kilikashifiwa kwa kuitwa Chama Cha NCCR-'Manunuzi' huku Dkt. Slaa akimtaka Bw. Mbatia kama anataka kutangaza majina ya Wabunge wa viti maalum CHADEMA, aombe Ukatibu MKuu wa Chama hicho.

"Namheshimu sana Dkt. Slaa lakini kitendo cha kusema kuwa mimi ndio nimesema Mdee ni Mbunge wa viti maluum akisahau kuwa yeye ndiye aliye tangaza na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi la Septemba 29 imenisikitisha sana" alisema.

Bw. Mbatia aliitaka CHADEMA kuitisha mkutano mahali palepale kwa watu walewale na kukanusha madai dhidi yake ndani ya siku tatu.

"Tumewapa siku tatu kuitisha mkutano wa hadhara, kama waliouitisha mwanzo, wakanushe uzushi huo vinginevyo tunawapeleka mahakamani" alisema.

Post a Comment

0 Comments