Poulsen Ataja kikosi cha Taifa Stars watakaovaana na Morocco

Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Jan Poulsen alitaja kikosi cha nyota 23 kwa ajili ya kuwakabili Morocco hapo Oktoba 9 huku akimrudisha kiungo mshambuliaji wa Simba, Mohammed Banka.Banka, nyota aliyeonyesha kiwango bora msimu uliopita akiisaidia Simba kutwaa ubingwa, ameitwa katika kiosi cha Stars kama mmoja wa washambuliaji chini ya Paulsen aliyeitwaa timu hiyo tangu Agosti 1 akichukua nafasi ya Mbrazil, Marcio Maximo.
Mara ya mwisho Banka kuitwa kikosi cha Stars, ni wakati timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Mzalendo, Dk. Mshindo Msolla aliyemwachia jukumu hilo Maximo kuanzia Julai, 2006 ambaye hadi anamaliza miaka minne Julai mwaka huu, Banka hajawahi kuitwa.Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mjini Morogoro, jana ambako timu yake ya Simba ilikuwa ikicheza na Mtibwa Sugar, Banka alisema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kuahidi kujituma vilivyo kuisadia timu hiyo na kusema anamshukuru Mwenyezi Mungu.Stars inakabiliwa na mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2012 ‘CAN 2012’ zitakazofanyika kwa pamoja nchini Gabon na Guine ya Ikweta.Katika mechi za kwanza katika kundi hilo la ‘D’ zilizochezwa Septemba 3 na 4, Stars ilivuna sare ya ugenini ya bao 1-1 huku Morocco ikiwa nyumbani ilitoka sare ya bila kufungana na Afrika ya Kati.Paulsen alisema katika uteuzi wake amezingatia kiwango cha nyota hao kwa mechi za hivi karibuni, hivyo anaamini vijana hao watadhihirisha ubora wao katika mechi dhidi ya Morocco.Alisema anafahamu ugumu wa mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, lakini watanzania hawana budi kutoa kila aina ya sapoti kwa timu hiyo ili iweze kuwafunga Morocco.Kiuchezaji, Paulsen alisema atatumia mfumo wa kujilinda zaidi na kupanga mashambulizi mara chache pale inapostahili kufanya hivyo kutegemeana na mbinu za wapinzani.Mbali ya Banka, Poulsen amewaita kwa mara ya kwanza nyota wengine watano, kipa Said Mohamed (Majimaji), Haruna Shamte (Simba), Salmin Kiss (Polisi Dodoma) na Salum Machaku (Mtibwa Sugar).Alisema kikosi hicho kitaingia kambini leo mchana, kitafanya mazoezi ya siku kadhaa kabla ya kuteua kikosi cha mwisho cha nyota 18 hapo Jumanne tayari kwa mechi ya Morocco.Poulsen alisema anaamini vijana wake watailetea timu hiyo mafanikio kwani wote wameitwa baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi za hivi karibuni, lakini akiwataka kuongeza juhudi.Alisema ni matarajio yake safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa na tatizo la kushindwa kutumia vizuri nafasi nyingi zinazopatikana, litaondoka ili kuwezesha timu kupata mabao.Kikosi kamili ni makipa: Shaban Kado (Mtibwa Sugar), Juma Kaseja (Simba) na Mohammed aliyechukua nafasi ya Jackson Chove.Mabeki: Shadrack Nsajigwa, Stephen Mwasyika (Yanga), Kiss (Polisi Dodoma) na Shamte (Simba), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Erasto Nyoni na Agrrey Moris kutoka Azam FC.Viungo: Henry Joseph (Kongsvinger, Norway), Shaban Nditi na Machaku (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz, Seleman Kassim (Azam FC), Nurdin Bakari (Yanga) na Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya) na Nizar Khalfan (Vancouver, Canada).Washambuliaji: Danny Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Banka na Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Mrisho Ngasa na John Bocco (Azam FC).Stars wanaingia kambini leo huku Morooco wakitarajiwa kutua Jumatano ijayo kwa ushauri wa Kocha Msaidizi, Mfaransa Dominique Cuperly kwa lengo la kuzoea hali ya hewa kabla ya mechi hiyo.

Post a Comment

0 Comments