Ya Kale Dhahabu

Enzi hizo Clyton wapili kushoto akiwa na bendi ya MK Group.
Hapa Cyton kushoto akiimba na Mutombo Odax. Kasongo Mpinda ‘Clyton’ wa kwanza kushoto hapa akiwa na wakongwe wenzake wa muziki katika enzi zao , ndiye muasisi wa MK. Group ‘Ngoma za Maghorofani’ enzi hizo.

Na Juma Kasesa
UNAPOZUNGUMZIA muziki wa dansi wa Tanzania na miongoni mwa wanamuziki waliosadia kwa kiwango kikubwa kuupa mashiko muziki huo huwezi kushindwa kumtaka Kasongo Mpinda ‘Clyton’.Mwanamuziki huyo mwenye asili ya mji wa Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) Lubumbashi lakini kwa sasa akiwa ni raia wa Tanzania anatajwa kuwa miongoni mwanamuziki walioweza kuubeba muziki wa dansi mwanzoni mwa miaka ya 1980 akitumia lugha adhimu ya Kiswahili. Alizaliwa 1945 akiwa ni mtoto familia ya watoto wanane elimu yake ni kidato cha kwanza akiwa anafuata nyayo za uimbaji kutoka mama yake mzazi ambaye alikua mwimbaji katika Kanisa Katoliki mjini Lubumbashi. Miongoni mwa nyimbo zilizoweza kumtambulisha katika medani ya muziki wa dansi wakati akitua nchini kutokea Zambia alikokuwa akifanya shughuli za muziki akiwa na bendi yake ya The Wings na kujiunga na Marquis ni ‘Angelou’, ‘Baharia’, na ‘Nasononeka’. Kwa wale wanaokumbuka enzi za Ukumbi wa Lang’ata Kinondoni jijini watakubaliana nami Kasongo aliiwezesha Marquis kupata mafanikio akiwa na wanamuziki wengine aliojiunga nao kutokea Zambia, Belly Kankonde na Kayembe Ndalambu na kuanzisha mtindo wa ‘Ogelea Piga Mbizi’ ambao ulikua ni ‘kijembe’ kwa wapinzani wao Ochestra Safari Sound. Uwezo wa kutunga na kuimba anataja kuwa ndiyo siri ya mafanikio yake iliyomuwezesha kung’ara akiwa na waimbaji wengine aliowakuta Marquis, ambao ni Kasaloo Kyanga, King Kiki, Parash Mukombole, Mbuya Makonga, Mtombo Odax Kiniki Kyato, mpiga solo mahiri Nguza Vicking chini uongozi wa Rais wa bendi hiyo Chinyama Chiyaza.Anawataja wanamuziki wengine aliokuwa nao enzi za Marquis kuwa ni wapiga Saxaphone, Mafumu Bilali ‘Bombega’, Kimeza Abdala, Bery Kankunde, huku Trumpet zikipulizwa na Kaumba Kalemba, Kayembe Ndalambu wakati gitaa la solo likivurumishwa na Nguza Vicking, Lubaba Ilunga na gitaa zito la besi likiwa chini ya Banza Mchafu.
“Nilianza muziki muda mrefu sana tangu mwanzoni mwa miaka ya 1965 nikiwa (Zaire) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo nikiwa na bendi mbalimbali kama Ode Jazz, Lupe Jazz kabla ya kujiunga na mkongwe wa muziki Dk. Nico Kasanda mjini Kinshasa,”anaeleza Kasongo na kuongeza. “Sikukaa sana na Dk. Nico ambapo 1968 nikaamua kuanzisha bendi yangu yangu ambayo ni The Wings Brother’s ambayo nilifanya nayo safari nchini Zambia, Malawi, Botswana na Zimbabwe kabla ya kutua Tanzania,”Mwanamuziki huyo licha kuanza shughuli za muziki muda mrefu, lakini ubora wa sauti yake tangu enzi na enzi upo palepale hali inayomuongezea heshima na funzo kwa wanamuziki wa sasa. “Unajua mimi nafuata miiko yote ya muziki ili kuepuka kupoteza sauti yangu ambayo ndiyo inaniwezesha kuishi na kuwakuna mashabiki hadi leo, jambo ambalo vijana wa sasa hawalifuati na kujikuta wakishindwa kudumu katika muziki muda mrefu,” anaeleza. Kasongo anaitaja Marquis kuwa ni bendi ambayo ilimsaidia kumuongezea ujuzi, umaarufu na kipato kutokana na kujizolea mashabiki lukuki kila mahala walipokuwa wakipiga kabla kujing’atua na kwenda kuasisi bendi ya MK. Group ‘Ngoma za Maghorofani’ iliyokuwa ikimilikiwa Mayaula Baraka Kaka yake na Asha Baraka 'Iron Lady'.
Anasema 1986 aliamua kutimka Marquis peke yake kabla ya wanamuziki wengine kumfuata na kujiunga na MK. Group kwa lengo la kujipima uwezo kama anaweza kuongoza bendi nchini na kujitafutia maslahi zaidi. Miongoni mwa wanamuziki waliokua wakiunda bendi hiyo ni Mbombo wa Mbomboka, Joseph Batholomeo Mulenga ambaye alikua raia wa Zambia, Kawele Mtimana, Sidy Moris, Asia Daruwesh, Kalala Mbwembwe, Kayembe Ndalambu na Mafumu Bilali. Kasongo anasema alishitushwa na namna mashabiki walivyoweza kumpokea kwa kishindo licha ya kujitoa Marquis, ambapo zawadi yao ya kwanza waliyowapa mashabiki ilikuwa ni nyimbo 6 kwa mpigo ambazo ni ‘Nishike Mkono’, ‘Kibela’ ‘Bibi na Bwana’, utunzi wake, ‘Nikale angara’ (Paulo Vitang) ‘Maria Maria’ (Sidy Moris) na ‘Adaria’ (Mbombo wa Mbomboka). “Niliona kama ndoto kwangu kukuta mashabiki walivyoweza kujazana New Africa Hotel, jambo ambalo liliniongezea hamasa ya kujituma na kutunga nyimbo zaidi nikishirikiana na wenzangu tuliokuwa nao tuliweza kupata mafanikio mwaka 1987 kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Top Ten kwa bendi za muziki wa dansi iliyokuwa ikiendeshwa na Redio Tanzania sasa TBC,”anasema Kasongo. Kwa wale wanaokumbuka wakati ule Top Ten ilikuwa ikiendeshwa na aliyekuwa Mtangazi wa (RTD) Julias Nyaisanga na wimbo ulioiwezesha MK. Group kutwaa ubingwa huo ilikuwa ni ‘Utakuja Kuanguka kwenye Matope’ ukiwa unaunga mkono kauli ya Rais Ally Hassan Mwinyi ya ‘Fagio la Chuma’. Anasema changamoto ambayo alikuta nayo katika kuingoza bendi hiyo, ni pale jopo la wanamuziki kadhaa walipojing’atua na kwenda kuasisi Tuncut Almasi lakini alisimama imara na kusaka wanamuziki wengine ambao walizidi kuijengea heshima MK Group, kabla ya bendi hiyo kusambaratika mwaka 1992 kutokana na kufungwa kwa Hotel ya New Africa Hotel baada ya Menejimenti kubadilishwa . “Baada ya kusambaratika kwa MK. Group niliamua kujiunga na Zaita Musica iliyokuwa chini ‘Maestro’ Ndala Kasheba ambapo tulifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kabla ya kukumbwa na misukosuko mingine ya kimuziki,”anaeleza. Mwanamuziki huyo ambaye ni baba watoto kadhaa anauzungumzia muziki wa zamani kama kioo cha vijana wa sasa kujifunzia kutokana na ubora wa tungo na mpangilio ulivyokuwa, tofauti na muziki wa sasa ambao huandaliwa na mtu mmoja jambo ambalo limepoteza dhana ya muziki ya kuelimisha na kuburudisha. Kwa sasa Kasongo anashirikiana na mkongwe mwingine wa muziki wa dansi Tshimanga Kalala Asosa wakiwa na bendi ya Bana Marquis wakitoa burudani sehemu mbalimbali za Jiji ambapo anatoa ushauri kwa wanamuziki ili waweze kupata maendeleo ni lazima wapendane na kushirikiana ili kufikia lengo la kujinufaisha kupitia muziki.

Post a Comment

0 Comments