TARI NA ICIPE ZAONGEZA NGUVU KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU WA MATUNDA

 


Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (icipe) cha nchini Kenya, zimeongeza kasi ya kusambaza teknolojia salama za Udhibiti Husishi wa Wadudu (IPM). Hatua hii inalenga kuokoa mazao ya parachichi, embe, na machungwa mkoani Kilimanjaro na Tanga, maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na uharibifu mkubwa wa nzi na nondo wa matunda.

Tafiti zinaonesha kuwa nzi wa matunda husababisha hadi 25% ya upotevu wa parachichi katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania, wakati nondo wa matunda akisababisha hasara ya karibu 40% kwenye machungwa.

Kwa muda mrefu, maeneo mengi yamekuwa yakitegemea matumizi makubwa ya kemikali; njia ambayo si salama kwa mazingira, afya ya walaji, na soko la matunda kama hazitatumika kwa usahihi.

Kupitia mradi wa Fruit Tree Agroecological-based IPM katika wilaya za Siha, Hai, na Muheza, wakulima wanafundishwa mbinu mbadala zinazolenga kukata mzunguko wa uzazi wa wadudu hawa na kupunguza matumizi ya viuatilifu vya kemikali.
Mbinu hizo ni pamoja na; Ukaguzi wa mara kwa mara wa mashamba, Matumizi ya mitego maalum ya kunasa wadudu, Matumizi ya vimeleatilifu hai (biopesticides), Matumizi ya mtego wa chambo cha protini (protein bait) ambao hutumiwa zaidi kudhibiti nzi wa kike wanaohitaji protini kwa ajili ya makuzi ya mayai yao. Njia nyingine ni usafi wa mashamba kupitia matumizi ya mahema maalum ya kuhifadhi matunda yaliyooza (augmentaria) ili kuzuia wadudu kuzaliana, na pia matumizi ya wadudu jamii ya nyigu aina ya Diachasmimorpha longicaudata (DL) na Fopius arisanus chini ya uratibu wa mamlaka husika. Mbinu hii ya kibaolojia inatumika kudhibiti nzi wa matunda (fruit flies) ambao wanaharibu maembe, machungwa, na parachichi, pamoja na baadhi ya mboga-matunda.
Ili kuhakikisha uendelevu wa mradi huu unaofadhiliwa na shirika la GIZ kupitia icipe, mnamo Septemba 27 na 28, 2026, jumla ya wakulima 259 wa Wilaya za Siha na Hai walipata mafunzo ya vitendo na kugawiwa mitego ya kunasa nzi wa matunda. Mafunzo hayo yalihusisha pia maafisa ugani na kampuni ya Elephant Vert ya mkoani Arusha, ambayo inazalisha na kusambaza mitego na vimelea tilifu. Lengo la kuwakutanisha wakulima na wasambazaji wa pembejeo ni kurahisisha upatikanaji wa vifaa na teknolojia hizo salama
Wakulima waliohudhuria wamepongeza juhudi hizo na kuomba watafiti kusogeza elimu hiyo kwenye kata ambazo bado hazijafikiwa.

Akitolea ufafanuzi hatua zinazofuata, Mtafiti Kiongozi wa mradi huo kutoka TARI, Dkt. Abdullah Mkiga amesema teknolojia hizi kila mkulima akizitumia ni rahisi kudhibiti changamoto ya wadudu waharibifu kwa upana zaidi (Areawide control). "Tunapanga kupanua wigo wa mradi huu ili tuwafikie wakulima wengi zaidi. Katika maeneo ambayo tayari tumeshafundisha, tumeona wakulima wameelewa na tumewaunganisha na wasambazaji wa pembejeo." Amesema.

Post a Comment

0 Comments