TMA IMETOA UTABIRI WA MVUA ZA VULI KWA KIPINDI CHA OKTOBA HADI DESEMBA 2026

Dar es Salaam. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi na wadau mbalimbali kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za msimu wa vuli zinazotarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Mwelekeo huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladslaus Chang’a, katika taarifa yake kwa Waandishi wa habari kuhusu muelekeo wa mvua za msimu wa vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026.

TMA imesema msimu huo unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Novemba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba katika Ukanda wa Ziwa Victoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba.

Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani ni pamoja na Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, kaskazini mwa Kigoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, kaskazini mwa Morogoro pamoja na Unguja na Pemba.

Dkt. Chang'a amesema tofauti na kawaida ambapo mvua za vuli huishia mwezi Desemba, msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi Januari 2027.

Katika Ukanda wa Ziwa Victoria, mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba na kuendelea hadi Januari 2027. Kwa upande wa Pwani ya Kaskazini, ikiwemo Dar es Salaam, Tanga na Pwani, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.

TMA imeonya kuwa wingi wa mvua unaweza kusababisha unyevu kupita kiasi kwenye udongo na mafuriko, hali inayoweza kuathiri mazao na miundombinu ya kilimo.

Aidha, ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linaweza kuathiri miundombinu ya maji na nishati, huku uchafuzi wa maji ukiongeza uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wa kilimo, wakulima wametakiwa kuandaa mashamba, kupanda na kutumia pembejeo kwa wakati, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia maji kutuama, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.

TMA pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa ya mifugo, yakiwemo homa ya bonde la ufa na kuoza kwa kwato, huku wafugaji na wavuvi wakishauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na ushauri wa wataalamu.

Katika sekta ya usafiri, mvua hizo zinaweza kuathiri barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege kutokana na mmomonyoko wa udongo, mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

TMA imesisitiza umuhimu wa wananchi na wadau kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, ikiwemo utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi, ili kuchukua hatua kwa wakati.

Aidha, imewataka waandishi wa habari kutumia taarifa rasmi zinazotolewa na TMA pekee na kuziwasilisha kwa lugha rahisi ili wananchi waweze kuelewa na kujiandaa dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa.

Post a Comment

0 Comments