Tarehe 18 Mei, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alimpokea Ikulu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake, Bw. Nathan Belete, aliyefika kumuaga Mheshimiwa Rais na kumtambulisha mrithi wake, Bw. Firas Raad.
Katika mazungumzo yao, Bw. Belete—aliyekuwa akisimamai Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, na ambaye sasa amepandishwa kuwa Mkurugenzi wa Programu za Kikanda wa Benki ya Dunia barani Afrika—pamoja na Bw. Raad, walizungumzia safari ya maendeleo ya Tanzania, matarajio ya nchi kwa siku zijazo, na mwendelezo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Katika mahojiano haya, Bw. Belete anaeleza uzoefu wake, mambo muhimu aliyojifunza na mtazamo wake kuhusu fursa za Tanzania kwa miaka ijayo, huku Bw. Raad akieleza matarajio yake na maeneo ya kipaumbele anapoanza majukumu yake nchini.
Bw.Nathqn Beletw Mkurugenzi Mkazi anayemaliza muda wake
Swali: Unapohitimisha kipindi chako cha miaka minne kama Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, ni mafanikio au hatua gani muhimu unazozikumbuka zaidi, hata sasa unapoanza jukumu jipya la kikanda barani Afrika?
Jibu: Ni heshima kwangu kufanya kazi Tanzania, nchi nzuri yenye watu wazuri, kote Bara na Zanzibar. Ni jambo lenye nafasi ya kipekee katika maisha yangu. Ninajivunia ushirikiano wetu na Serikali, wananchi na wadau mbalimbali nchini, kupitia programu kubwa inayogusa karibu sekta zote.
Katika kipindi changu, msisitizo ulikuwa zaidi kwenye sekta zinazogusa maendeleo ya watu, hususan elimu, afya na hifadhi ya jamii. Programu hizi zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Tunajivunia mchango wetu katika mageuzi ya sekta ya afya, ikiwemo bima ya afya kwa wote, pamoja na maboresho ya elimu, hasa mitaala ya shule za msingi na sekondari, na msukumo uliowekwa kwenye elimu ya ufundi na stadi.
Pia ninafurahishwa na mageuzi yaliyofanyika kwenye upande wa miundombinu, hasa katika sekta ya nishati.
Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia Tanzania ikipiga hatua kubwa katika upatikanaji wa nishati, halikadhalika katika sekta ya maji na huduma za usafi wa mazingira vijijini; na matarajio yetu ni kuona maeneo hayo yakiendelea kukua zaidi.
Swali: Tanzania inapojiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Julai 2026, ipi ni nafasi ya Benki ya Dunia katika kuunga mkono juhudi za kuwapa vijana na sekta binafsi wajibu mkubwa zaidi katika mageuzi hayo?
Jibu: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni fursa muhimu kwa Tanzania, ikichagizwa na mwelekeo wa Serikali kwa vijana katika kukuza ajira na sekta binafsi, kama msingi imara wa kuyafikia malengo ya Dira hiyo.
Kwetu sisi, Benki ya Dunia, tunaiona nafasi nzuri ya kuvutia mitaji zaidi ya sekta binafsi ili kusaidia miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo Reli ya SGR na maendeleo ya bandari.
Tunaamini haya yanawezekana, kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye msingi wa uchumi imara barani Afrika, na mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi.
Kwa sababu hiyo, mageuzi katika mazingira ya biashara na uwekezaji ni muhimu. Mengi yamefanyika, lakini bado kuna nafasi zaidi ya kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi nchini.
Rasilimali za Tanzania zinaipa nchi nafasi ya kipekee, si kwa ukuaji wake pekee, bali pia kwa maendeleo ya nchi jirani na kanda pana ya Afrika.
Nafasi ya Tanzania kama kiungo cha nchi nane zinazopakana nayo ni faida kubwa ya kuendelezwa. Kwa mtazamo wangu, hili ni suala muhimu sana.
Namna tunavyotazama umuhimu wa vijana stereotypes na nafasi yao katika maendeleo, tunagusa moja ya malengo makuu ya Benki ya Dunia barani Afrika, ambalo ni kutengeneza ajira kwa vijana.
Nadhani njia hizi zinaweza kuwa msingi mzuri wa kutengeneza ajira, sambamba na mageuzi ya mitaala ya elimu ya ufundi ambayo tayari Tanzania imekwishaanza, yatasaidia kuwapatia vijana ujuzi na fursa bora zaidi za ajira. Hili ni jambo muhimu sana kwa utengamano wa si tu Tanzania pekee, bali bara zima la Afrika
Swal: Zaidi ya utajiri wa rasilimali za asili na utulivu wa kiuchumi, ni mambo gani mengine yanayoifanya nchi ya Tanzania kuwa ya kipekee katika ukanda huu?
Jibu: Tanzania ipo katika nafasi nzuri na ya kipekee ya ukuaji wa uchumi barani Afrika. Ni nchi yenye utulivu, inayosimamia deni kwa umakini, na kutumia rasilimali zake kwa weledi. Hata hivyo, bado kuna mwanya wa kufanya zaidi, na kazi hiyo inaendelea. Katika majadiliano yetu kuhusu ufadhili wa Benki ya Dunia, tumeshuhudia umakini wa Tanzania katika matumizi bora ya rasilimali zilizopo.
Suala la msingi kwa sasa, ni mwelekeo wa kupunguza utegemezi wa miradi inayofadhiliwa na sekta ya umma, na kuongeza miradi inayofadhiliwa na sekta binafsi.
Jitihada hizi ni muhimu pia katika kuimarisha usimamizi wa miradi, iwe ya sekta ya umma au binafsi; na niseme tunathamini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika eneo hili.
Swali: Katika kipindi ulichofanya kazi Tanzania, ni mambo gani muhimu umejifunza utakayayaishi katika jukumu lako jipya la uongozi barani Afrika?
Jibu: Mara kadhaa tumekuwa tukisema suala la utekelezaji ni changamoto kubwa barani Afrika; lakini Tanzania, kwa mtazamo wangu, imeonesha kuwa sekta ya umma inaweza kufanya kazi vizuri ikijizatiti.
Tumeshuhudia baadhi ya miradi yetu kutofanya vizuri katika baadhi ya sekta, lakini pia tumeona matokeo makubwa katika sekta na wizara nyingine.
Niliyoyaona Tanzania katika sekta ya nishati, maji vijijini, pamoja na huduma za usafi wa mazingira yanavutia sana. Nchi hii imeonesha kuwa utekelezaji wa miradi katika sekta muhimu na kuleta matokeo kwa wananchi, ni suala linalowezekana.
Ningependa kuona kasi hii ya utekelezaji ikiendelea, kwa sababu Tanzania imeonesha kuwa hilo linawezekana pale kunapokuwa Greeting na dhamira na utayari kisiasa, kiutendaji, na uratibu kati ya wadau na jamii. Hili ni moja ya masomo makubwa ninayoondoka nayo, na ninatumaini Tanzania itaendelea kuimarisha uwezo wake wa utekelezaji katika wizara zote.
Swali: Kwa mtazamo wako, ni katika eneo lipi Tanzania inaweza kuweka msisitizo zaidi ili kuongeza kasi ya maendeleo na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi wengi kwa muda mrefu?
Jibu: Kuna maeneo machache ambayo, kwa mtazamo wangu, yanahitaji kuendelea kupewa msisitizo. Kwanza, kunahitajika umakini zaidi katika ushirikishwaji wa wananchi kwenye usanifu na utekelezaji wa programu mbalimbali.
Lakini pia panapaswa kuwa na uwazi na ufanisi zaidi katika ushirikishwaji wa sekta binafsi. Mwisho, jitihada za kuimarisha utawala bora zinapaswa kuendelezwa katika sekta zote, ili kulinda maslahi ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Swali: Kama Mkurugenzi Mkazi mpya wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, ni vipaumbele na fursa gani unazoziona katika hatua inayofuata ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania?
Jibu: Leo, (Benki ya Dunia) tumepata heshima ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kujadili mtazamo na matarajio yetu kuhusu mustakabali wa ushirikiano wetu.
Nilieleza pia mtazamo wangu kuhusu kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania na utulivu wa uchumi kwa ujumla. Mambo haya mawili ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta binafsi tunayoyaona. Na ni maeneo ambayo kimsingi tutaendelea kuyapa kipaumbele.
Kwa upande wetu sisi Benki ya Dunia, na hili tulilieleza kwa Mheshimiwa Rais, pamoja na viongozi wa Serikali, ajenda ya ukuaji wa uchumi na ajira ni suala muhimu sana.
Ili kufikia azma ya kupunguza umaskini kwa ufanisi, tunahitaji si tu kukuza uchumi, bali pia kutengeneza ajira. Hili litasaidia kufikia lengo la kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya Watanzania wote.
Katika kufanikisha hilo, hatuna budi kuweka mkazo katika miundombinu ya msingi, yaani miundombinu ya watu na vitu; ambayo ni elimu, hifadhi ya jamii, na afya, pamoja na nishati, usafiri na mengineyo. Hili, kwa mtazamo wangu, ni eneo muhimu sana.
Eneo la pili ni kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara, jambo ambalo Tanzania imeendelea kulifanyia kazi. Tunatarajia kuendelea kushirikiana na Serikali, Tanzania Bara na Zanzibar, katika kujenga mazingira yatakayovutia uwekezaji unaohitajika kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Na mwisho, ni eneo ambalo Mkurugenzi anayemaliza muda wake pia amelipa msisitizo, nalo ni kutumia mtaji wa sekta binafsi kuchochea maendeleo. Tunahitaji nguvu zaidi kuiunga mkono Tanzania ili iweze kuvutia mtaji wa sekta binafsi katika maeneo muhimu yanayoweza kubadili uchumi wa nchi.
Kama mnavyofahamu, nafasi ya fedha za umma kugharamia mahitaji ya maendeleo imeendelea kuwa finyu. Ndiyo maana ni muhimu mtaji wa sekta binafsi uingie kuongeza nguvu katika maeneo ambayo Serikali haiwezi kuyagharamia peke yake.
Kwa hiyo, matarajio yetu ni kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania, kupanua na kuimarisha ushirikiano huu, huku tukihakikisha unaendelea kujikita katika maendeleo yanayomgusa mwananchi moja kwa moja.
Ninatarajia kuendeleza ushirikiano huu katika jukumu langu jipya kama Mkurugenzi wa Benki ya Dunia, ninayeisimamia si Tanzania pekee, bali pia Malawi, Zimbabwe na Zambia.
Swali: Ni kwa namna ipi Benki ya Dunia inaweza kusaidia Tanzania na ukanda huu kwa ujumla kuimarisha rasilimali watu, na kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaohitajika katika uchumi wa siku zijazo?
JIBU: Kama mnavyofahamu, elimu ni sekta muhimu sana. Ni moja ya maeneo ambayo uwekezaji wake huleta matokeo makubwa, ingawa matokeo hayo huonekana zaidi katika muda wa kati na mrefu.
Kwa hiyo, tunahitaji kuwekeza sasa ili kuona matokeo bora ya ujifunzaji katika miaka mitano hadi saba ijayo. Kwahiyo, Benki ya Dunia inawekeza zaidi katika maendeleo ya watu, hususan elimu, hifadhi ya jamii na afya.
Mtakumbuka kuwa, miaka michache iliyopita, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Rasilimali Watu, uliochangia kuweka msisitizo mkubwa katika eneo hili na kuonesha nini kinaweza kufikiwa. Bado kuna mapengo makubwa katika nchi nyingi barani Afrika, lakini kupitia uwekezaji katika elimu, afya na hifadhi ya jamii, tunaweza kuanza kuyapunguza.
Jambo lingine muhimu ni ujuzi unaohitajika kwa ajili ya nguvu kazi ya siku zijazo. Hatuwezi kuzisaidia nchi kukuza uchumi, kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya wananchi bila kuboresha matokeo ya ujifunzaji na ujuzi wa nguvu kazi. Hili pia ni eneo tunalotarajia kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania, pamoja na Serikali nyingine katika ukanda huu.
Swali: Na je, katika kipindi cha muda mfupi, mambo yapi yapewe kipaumbele?
Jibu: Katika kipindi cha muda mfupi, tunaweza kuongeza uwekezaji katika afya na hifadhi ya jamii, kwa sababu ni muhimu kulinda rasilimali watu. Kama mnavyofahamu, nchi nyingi barani Afrika mara kwa mara hukumbwa na misukosuko kutoka nje, iwe ni athari za tabianchi au changamoto za kiuchumi, kama tunavyoona sasa kutokana na mgogoro wa Mashariki ya Kati. Hivyo, tunahitaji kuhakikisha uchumi wetu, na hata kaya zetu, zina uwezo wa kuhimili changamoto hizo.
Hili linawezekana kupitia mifumo ya kisasa ya hifadhi ya jamii na upatikanaji wa huduma bora za afya. Katika maeneo haya, tunajivunia kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania



0 Comments