Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesifu msimamo wa watanzania kwa kuwapuuza mamluki na vibaraka wachache wanaotumiwa na mabeberu kuvuruga ustawi wa amani, umoja na mshikamano wa kiTaifa.
Kimekitaja kitendo cha wananchi kuonyesha utii wa sheria na kutojitokeza katika maandamano haramu ya 09 Desemba 2025, kimefikisha ujumbe kuwa waTanzania kamwe hawatagawanyika
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo na kuwataja waTanzania walikataa, wamekataa na wataendelea kukataa kuuza utu wao au kupoteza heshima ya Taifa lao.
Mbeto aliwashukuru waTanzania kwa uamuzi huo unaodumisha amani na utulivu, ukiwasuta vibaraka wanaonunulika kwa ujira wa fedha zenye dhambi ili wachochee machafuko nchini.
Alisema njia pekee bora na sahihi ni serikali kuendelea na mkakati wake wa kuzitafutia tiba changamoto zinazowakablii wananchi, kuboresha huduma za jamii na kupata mbinu mbadala zitakazotanua wigo wa ajira kwa vijana.
"Watanzania kwa umoja na mshikamano wao wamewatumia ujumbe vibaraka wachache waliodhani wangefanikiwa kuwagawanya.
Kwa nguvu ya uzalendo, uTaifa walionao, wamechagua kulinda heshima na kukataa kugawanyika" alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema kwa namna yeyote ile, waTanzania wataendelea kuthamini Taifa lao, umoja wa kitaifa wa nchi zao kwani wamekuwa wakiishi kwa maelewano kwa miaka zaidi ya sitini.
"Ahadi na kazi ya CCM ni kuzisukuma serikali zitekeleze wajibu wa kisera kwa kuzipatia majibu chanya changamoto zote. CCM iko tayari wakati wowote kumaliza utata wowote kwa njia ya majadiliano na mazungumzo mezani "alisema.
Alimtaja Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi shupavu, msikivu, muungwana, anayeshaurika hivyo yuko tayari wakati wowote kushughulikia matatizo kwa njia za kistaarabu.
Katibu huyo Mwenezi aliwataka waTanzania kusoma mienendo hatarishi iliozikumba na inayoendelea kuzitatiza baadhi ya nchi na mizozo yake imeacha vita, mapigano na machafuko yasiokwisha.
"Watanzania tukatae ghiliba na ushawishi utakaovuruga amani na utulivu. Tuwe tayari kujadili changamoto kwa njia za wazi bila kuvutana mashati. Thamàni ya amani, umoja na utulivu haiuzwi mahali popote duniani " alisema Mbeto.

0 Comments