UKICHEPUKA NJE YA NDOA UNAUAWA KWA WAHADZABE.

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.

Jamii ya kabila la Wahadzabe inayopatikana pembezoni mwa Ziwa Eyasi Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha ni miongozi mwa makabila yaliyopo katika mzunguko wa Jiopaki ya Ngorongoro Lengai.  Jamii hii ni wanufaika wa mradi wa makumbusho mpya ya kijiolojia (Urithi Geopark) iliyopo katika mji wa Karatu.

Nchi ya Tanzania na barani Afrika kwa ujumla zipo kanuni na taratibu mbalimbali ambazo jamii au makabila hujiwekea kama njia ya kuenzi na kutunza mila na desturi zao.

Katika kabila la Wahadzabe (Watindiga) kwa wanandoa (mke na mume) kufanya tendo la ndoa na mtu mwingine  nje ya ndoa (Kuchepuka) inatafsiriwa kuwa ni laana kubwa kwa kabila hilo ambapo mtu anayefanya kosa hilo na ikathibitika adhabu yake ni kuuwawa na mtu aliyewafumania (aliyewashuhudia) kisha akishatekeleza mauji anapiga ukunga au yowe ili jamii ikusanyike  na wazee wa kimila kutoa taarifa rasmi kwa jamii kuhusu kitendo hicho ambacho kinatafsiriwa kuwa ni kuleta laana na nuksi kwenye familia. 


Njia inayotumika kuwaua waliochepuka ni kuchomwa na mishale yenye sumu mwilini Mithili ya mnyama anayewindwa, Mishale inayotumika ina sumu kali ambayo huenea haraka kwenye mwili  wa mwanadamu na kupoteza maisha ndani ya muda mfupi.

Katika maisha ya mapenzi na ndoa kwa jamii ya wahadzabe zipo kanuni mbalimbali  ambazo wamejiwekea ikiwemo kila mwanaume anayeoa na mwanamke anayeolewa kuheshimu ndoa yake na kuepuka kwa vyovyote vile kushiriki tendo la ndoa na mwanamke au mwanaume mwingine.

Baada ya kuoana bibi na bwana harusi hutakiwa kuishi kwa upendo na jamii hufuatilia ndoa hiyo ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu miongoni mwao anayefanya tendo la ndoa nje ya mwenza wake, jamii hiyo ipo makini katika kufuatilia mienendo ya wanandoa ili kuhakikisha kuwa usalama wa familia unakuwepo katika kipindi chote cha ndoa hiyo.

Mchakato wa kuwaua wanandoa waliochepuka haufanyiki kwa kukurupuka bali uchunguzi na ufuatiliaji wa kina hufanyika mpaka pale watu wanaoaminika watakapowashuhudia watuhumiwa wakiwa katika kilele cha ndoa hiyo.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Mila za Wahadzabe Mzee Shagembe Gambai Jamii hiyo imeweka utaratibu huo wa kuwaua watu wanaochepuka ili kuimarisha nidhamu za familia, ukoo na jamii kwa ujumla ndio maana hadi sasa utaratibu huo umezoeleka na kuheshimiwa hivyo ni nadra sana kusikia mhadzabe akichepuka.

Katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anajifunza ubaya wa kuchepuka zoezi la kuwaua waliofumaniwa hufanyika hadharani likishuhudiwa na jamii yote ya eneo hilo wakiamini kuwa kitendo hicho kinatoa darasa kwa wanandoa wengine kuacha tabia hiyo.


 Mzee Shagembe anasimulia kuwa Ndoa kwa jamii ya wahadzabe si suala la kufa na kuzikana laah hashaa, jamii hiyo huruhusu kuachana na ikitokea hivyo unaruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu mwingine hata kama huyo unayeanza naye uhusiano upya ni mtu wako wa karibu au rafiki wa aliyekuwa mwenza wako.

Jamii ya Wahadzabe hawaamini katika ndoa za mke zaidi ya mmoja, Kwao ndoa ya mke na mume mmoja tu na hairuhusiwi mwanaume kuoa mke zaidi ya mmoja sababu kubwa ikiwa ni kuimarisha upendo kwa wale walioamua kuishi kama mke na mume.

Post a Comment

0 Comments