Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimewaasa Viongozi wa dini kuacha kuvaa viatu vya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kulipoteza Taifa katika dira na ramani yake ya umoja, udugu na amani.
Pia chama hicho kimesema uamuzi wowote wa vongozi hao kuingilia siasa si katika jambo lenye tija nyakati zote.
Katibu wa Kamati Maalum vya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis alisema hayo katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Visiwani, Zanzibar.
Mbeto alisema matatizo yaliochomoza yana taswira ya siasa hivyo ni busara utatuzi wake ukachwa mikononi mwa saerikali na wanasiasa huku viongozi wa dini wakisubiri kushirikishwa itakapohitajika.
Alisema hata inapozuka mizozo au mitafaruku ya kidini kanisani kwenye mahekalu na misikitini, wanasiasa hawana nafasi ya kushiriki katika kufikia utatuzi ni busara pia kwa viongozi wa dini kutoingilia siasa.
"Viongozi wa serikali hawajachoka kutafuta Suluhu na utatuzi kwa yaliotokea. Si vyema na wala si ustaarabu viongozi wa dini kuwapangia hatma viongozi Serikali lipi la kufanya "alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi , alisema inasikitisha kuona viongozi wa dini kuu, Uislam na Ukristo, wakianza kuzungumzia masuala ya kisiasa ndani ya nyumba za ibada kwa jazba na hamaki .
'Taifa linaoongozwa na Serikali ya Rais , Mkuu wa Nchi mwenye mamlaka kisheria na kikatiba. Hajashindwa kumaliza yaliojitokeza. Ikiwa viongozi wa Dini watahitajika wataitwa kutoa ushauri itakapobidi " aibainisha Mbeto.
Alisema kwa namna yoyote ikiwa viongozi wa dini wataendelea kutoa matamko yenye hofu na taharuki katika jamii, Taifa linaweza kupitishwa katika Jangwa la hatari nyeusi isioepukika.
"Mwalimu Julius Nyerere amewahi kutamka hadharani Serikali ya Tanzania haina Dini. Wananchi ndiyo wenye imani za Dini. Hivyo si vyema baada ya miaka 60 Dini zijibebesha dhamana za kisiasa" alisema.
Mwenezi huyo aliongeza kusema Viongozi wa Dini wasiendelee kutoa matamko ya kuisakama Serikali kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa hawajengi mustakabali chanya wa taifa letu.
"Inapozuka mivutano ya dini huwa haina msalie wala sumile. Milipuko na vurugu zake huwa si kidogo kama inavyodhaniwa. Chonde jazba zisilipitishe Taifa katika bahari ya damu" alisema.
Hata hivyo Mbeto alisema misuguano iliowahi kutokea nchini kati ya Serikali ya chama tawala na Upinzani, ilimalizika kwa njia ya mazungumzo mezani bila kupata shinikizo toka mahali popote .

0 Comments