MBETO : HAKUNA USHURU MARA MBILI TOKA ZANZIBAR

 

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimebainisha kuwa hakuna kodi mara mbili zinazotozwa kwa bidhaa kutoka Zanzibar kuna upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na wanahabari Kisiwandui, Unguja, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Mafunzo, Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis alisema sio kweli, suala hilo linapotoshwa.

Alisema ACT Wazalendo ndio wanaongoza upotoshaji huo na kubainisha kuwa kuna Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZARA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kila moja ina majukumu yake.

Alisema pesa inazokusanya ZARA ni kwa ajili ya Zanzibar na haziendi TRA wala mamlaka zingine na kwa kuwa ina uchumi mdogo hivyo kuna ahueni kwenye kodi za bidhaa zinazoingizwa. 

 “Mathalan Zanzibar ushuru wa kuingiza gari shilingi milioni mbili lakini gari lile kwa Tanzania Bara TRA wanatoza shilingi milioni tano hivyo ukitaka kulivusha utaongoza milioni tatu ili kufikia viwango vyao TRA” alisema.

Alibanisha kuwa huo sio ushuru mara mbili isipokuwa hizo ni mamlaka mbili tofauti zinazojitegemea na wale ambao wanadai kuwa eti Zanzibar haina mamlaka kwenye Muungano, wameishiwa hoja.

“Wenzetu hoja zao chuki, ubaguzi na Muungano wasichokijua, Zanzibar ina upekee katika mambo yake ya ndani na Muungano na ndio maana inapata fursa mbili za mikopo kwa wakati mmoja” alisema.

Alizitaja fursa hizo ni pamoja na kuwa na uwezo wa kukopa fedha kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi (SMZ) kwa benki na taasisi za fedha za ndani.

Mbeto alidai kuwa ACT inaongozwa na chuki za kisiasa na kwa kudai kuwa Zanzibar haina mamlaka kwenye Muungano jambo ambalo si kweli kwani mapato yote yanayokusanywa na ZARA yanabaki Zanzibar. 

Upande mwingine Mbeto alisema CCM kinalaani matendo ya utekaji yanayojitokeza na kimewataka wananchi kuacha jukumu la uchunguzi kwa vyombo vya nje na ndani ambavyo vinayafanyia kazi matukio hayo.

Mwenezi Mbeto, alisema chama chake cha CCM kinaongozwa na katiba ambayo inataja kuwa kila mmoja anastahili haki, heshima na kulindiwa utu wake.

Alibainisha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kila raia kustahili haki zake, heshima na kulindiwa utu wake na CCM inaamini katika mazungumzo.

Alisema Mbeto kuwa ndio maana Rais Dkt. Samia Hassan alipoingia madarakani kuna wanasiasa aliwafutia kesi zilizokuwa zinawakabili mahakamani pamoja na watu wengine.

“Kina Mbowe walikuwa na makesi chungu nzima lakini aliamua kuzifuta na kuitisha mazungumzo” alisema na kuongeza kuwa utekaji una sura nyingi na si vema kuwasingizia viongozi wakuu wa serikali.

Aliwaasa vijana na watu wengine kuacha kuwatusi viongozi wa juu wa serikali mitandaoni na kwenye majukwaa ya siasa kwani huo sio utamaduni wa kiTanzania kwani Dkt. Samia katoa fursa ya mazungumzo katika kila jambo.

”Leo utanisema vibaya mimi Mbeto, lakini mimi sio watu wote wanaonichukia wapo wanaonipenda wanaweza wakaamua kuwa na visasi na pia viongozi wana ndugu, jamaa, watoto hivyo si jambo zuri kuwatusi kwenye mitandao na majukwaani” alisema.

Alisema tofauti na siasa kuna maisha nje ya siasa na watu wana wenzao wanaofanya nao biashara na wanaweza kutofautiana huko yakatokea mambo kama hayo kwa kuwa alikuwa mkosoaji wa serikali moja kwa moja wanawahusisha viongozi jambo ambalo sio sahihi.

“Sio jambo jema tuache mamlaka husika zifanye kazi zao kwani uchunguzi unafanywa si na vyombo vya ndani pekee bali pia vya nje vinafuatilia hivyo tuwe na subira wakikamilisha kazi yao watabainisha ukweli ulivyo.

Post a Comment

0 Comments